Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesema kipo kwa ajili
ya Watanzania kunufaika na fursa za uwekezaji zinazotokana na mageuzi makubwa ya uchumi na
teknolojia, ambayo yamechangia kuongezeka kwa kasi ya uwekezaji nchini.
Hayo yameelezwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa TIC,
Gilead Teri wakati akizungumza na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari leo
jijini Dar es Salaam, kuelezea mafanikio yaliyofikiwa na kituo hicho.
“Kasi ya kukua kwa uwekezaji Tanzania ni kubwa na TIC ipo
kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania kunufaika na fursa zinazotokana na mageuzi
makubwa ya uchumi na teknolojia, “amesema Teri na kuongeza, “Hata sasa, idadi
ya wawekezaji wa ndani wanaosajiliwa ni kubwa kuliko wakati wowote. Tumesajili
asilimia 49 wawekezaji wa ndani na asilimia 33 wa nje”.
Amesema mafanikio hayo yametokana na Tanzania kuwa na mazingira
mazuri zaidi ya uwekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine za ukanda wa Afrika
Mashariki na SADC kutokana na gharama za uzalishaji kuwa chini zikiwamo za
umeme.
Aidha Teri amesema katika kipindi cha Januari 2021 hadi Juni
2023, Kituo Kimesajili jumla ya miradi 778, ambapo mwaka 2021 kilisajili miradi
256 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 3,786.75 ambayo inatarajiwa
kuzalisha ajira 52,846.
Mwaka 2022 kituo kilisajili miradi 293 yenye thamani ya dola
za Marekani milioni 4,537.70 inayotarajiwa kuzalisha ajira 40,889 na mwaka huu
wa 2023 kuanzia Januari hadi Juni, kituo kimeshasajili miradi 229 yenye thamani
ya dola za Marekani milioni 2,208.14 na inatarajiwa kuzalisha ajira 31,647.
Usajili huo wa Miradi kuanzia Jan 2021 - Juni 2023 umekuwa
na manufaa kwa taifa kupunguza tatizo la ajira kwa kutengeneza ajira mpya
125,382, thamani ya miradi hiyo ni dola za kimarekani milioni 10,532 ambapo
mitaji kutoka nje na ndani imewekezwa.
0 Maoni