MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inatumia
maonesho ya 47 ya kimataifa ya kibiashara yanayoendelea Jijini Dar es Salaam
kuhamasisha umma wa watanzania wawekezaji na wageni kutoka mataifa mbalimbali
kuwekeza katika maeneo inayoyasimamia huku ikijinasibu kuwa na fursa lukuki za
uwekezaji.
Akiongea na wageni waliotembelea banda la TAWA lililopo ndani
ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii Afisa Mhifadhi Gregory Kalokole
amesema TAWA ina uwanda mpana wa fursa za uwekezaji unaotoa mwanya kwa
wawekezaji wa aina mbalimbali kuwekeza katika taasisi hiyo.
Akizitaja fursa hizo Kalokole amesema yapo maeneo mengi
yanayohitaji wawekezaji na uwekezaji katika taasisi hiyo kama vile maeneo ya
utalii wa picha kwenye maeneo ya hifadhi za Wanyamapori, maeneo ya kihistoria
yenye Utalii wa kiutamaduni, eneo la uwekezaji mahiri (Special Wildlife
Investment Concession Areas – SWICA), Uwindaji wa Kitalii na Ufugaji wa
Wanyamapori.
“TAWA imetenga maeneo kadhaa Kwa ajili ya kufanyika shughuli
za utalii wa picha kutokana na ikolojia na aina ya vivutio vilivyopo katika
maeneo hayo ikiwemo Pori la Akiba Mpanga/Kipengere eneo ambalo lina maporomoko
ya maji zaidi ya 10 ambayo hutoa burudani safi Kwa watalii,” amesema Kalokole.
“Mapori mengine ya Akiba ni Pande, Wamimbiki, Swagaswaga na
Kijereshi ambapo wananchi wanakaribishwa kuwekeza kwenye miundombinu ya Utalii
ikiwemo kujenga Kambi za Kulala wageni, hosteli, loji na maeneo ya mapumziko
mafupi (Picnic Sites),” ameongeza Kalokole.
Kwa Upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja ametumia
fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda la TAWA Ili kupata
maelezo ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi hiyo.
“Hii ni fursa adhimu Kwa wawekezaji wote kutembelea banda
letu ili waweze kupata ufafanuzi wa fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo
katika taasisi yetu kwani TAWA ni sehemu sahihi Kwa uwekezaji na wawekezaji,“
amesema Maganja.
Maonesho haya yenye Kauli Mbiu “Tanzania ni Mahali Salama Pa
Biashara na Uwekezaji” yameanza 28 Juni, 2023 na yanatarajiwa kufikia tamati 13
Julai, 2023.
Na: Beatus Maganja, Dar es Salaam.
0 Maoni