WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Nishati
iratibu ununuzi wa mafuta kutoka mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa ili
yachukuliwe kutokea Tanga badala ya Dar es Salaam.
Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Julai Mosi, 2023) mara baada
ya kukagua uboreshaji wa bandari ya Tanga na hifadhi ya mafuta kwenye matenki
ya GBP, eneo la Raskazoni, jijini Tanga.
"Mikoa ya Mara, Mwanza, Manyara, Arusha, Kilimanjaro
inafuata mafuta Dar es Salaam sababu ya mazoea lakini upatikanaji rahisi ni
hapa Tanga, upatikanaji wa haraka sababu ya teknolojia ni hapa Tanga. Wizara ya
Nishati watekeleze maelekezo haya ili wauzaji wa mafuta wayafuate Tanga,"
amesema.
Waziri Mkuu amesema endapo makampuni yote ya mikoa ya
Kaskazini yatachukulia mafuta Tanga, uchumi wa mkoa huo utakua kwa haraka.
Akielezea kuhusu uwekezaji kwenye hifadhi hiyo, Waziri Mkuu
amesema uwekezaji uliofanyika ni mkubwa kwani matenki yaliyopo yanaweza kupokea
mafuta moja kwa moja kutoka bandarini na kuhifadhi lita hadi milioni 200. “Huu
ni mkakati wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuendeleza uchumi wa nchi
yetu. Wakati Serikali inaongeza uwezo wa kusimamisha meli zaidi bandarini,
tutahakikisha kuwa uwekezaji huu unaleta faida kwa mwekezaji na unaongeza ajira
kwa wanaTanga,” amesema.
Mapema, akitoa taarifa kuhusu hifadhi ya matenki ya GBP,
Mkurugenzi Mtendaji wa GBP, Bw. Badar Sood alisema ujenzi wa matenki hayo
ulianza mwaka 2002 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 25 huku wakipokea
meli zenye uwezo wa lita 6,000 tu.
"Hivi sasa tunaweza kuhifadhi lita milioni 200, tunaweza
kupokea bidhaa mbili kwa wakati mmoja. Tunapokea hadi meli zenye ujazo wa lita
70,000 na tunaweza kupakia lita milioni tano hadi sita kwa siku kwenye malori
na kupakia mabehewa 20 kwa wakati mmoja ndani ya saa tatu,” amesema Bw. Badar.
Akiwa kwenye bandari ya Tanga, Waziri Mkuu alipokea taarifa
ya uboreshaji wa miundombinu na kuelezwa kuwa ujenzi wa gati mpya umekamilika
kwa asilimia 99 na kwamba zimebakia kazi ndogo za kukamilisha mifumo ya umeme.
“Uboreshaji wa bandari ya Tanga hadi sasa umegharimu sh.
bilioni 429.2. Awamu ya kwanza ulihusisha uchimbaji wa eneo la kuingilia meli
na kugeuzia lenye urefu wa km.1.7 na upana wa mita 75 kwa kina cha mita 10 na
awamu ya pili ni kujenga gati yenye urefu wa mita 450,” alisema Naibu
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavaro.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametembelea kiwanda cha
saruji cha Maweni na kupokea taarifa ya ujenzi wake unafanywa na kampuni ya
HUAXIN ya China.
Akizungumza na watumishi wa kiwanda hicho na wananchi
waliofika kiwandani hapo , Waziri Mkuu alimhakikishia Meneja Mkazi wa kampuni
ya Maweni Limestone Ltd, Bw. James Jing kwamba atapata makaa ya mawe ya kutosha
kadri ya mahitaji yake.
0 Maoni