Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania - TANAPA limejipanga kukusanya mapato kupitia vyanzo vyake vya ndani kiasi cha Shilingi Bilioni 343.8 katika mwaka wa fedha 2023/2024 tofauti na mwaka jana ambapo ilikusanya shilingi bilioni 337.
Akitoa taarifa hiyo katika mkutano na wanahabari ulifanyika
katika Ukumbi wa Idara ya Habari - Maelezo jijini Dodoma juu ya mwelekeo wa
Shirika hilo katika kukuza shughuli za Utalii kwa mwaka wa fedha 2023/2024,
Kamishna Mwakilema amesema "TANAPA imeweka mikakati thabiti ya kuongeza
idadi ya watalii kufikia 1,802,460 kwa mwaka 2023/2024".
Kamishna Mwakilema alisema, "shirika lina dhamana ya
kusimamia na kuendeleza maeneo yaliyoteuliwa kuwa hifadhi za taifa hivyo TANAPA
imeweka vipaumbele katika maeneo ya uhifadhi, ulinzi, utalii, ushirikishaji
jamii na uboreshaji wa miundombinu pamoja na ukamilishaji wa miradi ya
kimaendeleo ya shirika ili kufikia malengo tuliojiwekea".
Aidha, shirika limejipanga kuboresha miradi ya maendeleo kwa
ukarabati wa viwanja vya ndege katika Hifadhi za Taifa za Ruaha, Mikumi na
Nyerere, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege na Helikopta ili kuimarisha utalii
pamoja na shughuli za ulinzi mkakati.
Hata hivyo, Kamishna Mwakilema alisema, "shirika
limeendelea kujipanga katika kuboresha miradi ya maendeleo kwa kutenga bilioni
60.6 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ili kuwezesha utekelezaji wa maendeleo katika
miradi mbalimbali inayosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA)".
Sanjari na utekelezaji wa mipango hiyo itakayoweza
kuimarisha uchumi kwa shirika na taifa kwa ujumla TANAPA pia, imejipanga
kumaliza changamoto za uhifadhi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za
uhifadhi na serikali kwa kufanya kazi kwa weledi ili kumaliza migogoro ya
wanyamapori wakali na waharibifu.
Naye, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alitoa shukrani
kwa shirika kutoa ufafanuzi juu ya muelekeo wa TANAPA mbele ya wanahabari hao
ambao utawaongezea uelewa kutoa taarifa sahihi zinazohusiana na ulinzi wa
hifadhi za taifa na kuwa mabalozi wazuri wa kuvitangaza vivutio vya utalii kwa
wananchi na namna shirika hilo linavyofanya kazi zake kwa weledi na maarifa.
‘’Nikushukuru sana Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA kwa taarifa
yako yenye malengo chanya ya kukuza utalii na iliyotilia mkazo suala zima la
uhifadhi wa maliasili. Hivyo ni matumaini yangu kuwa wanahabari hawa wameelewa
dhana nzima ya uhifadhi wa vyanzo vya maji hivyo kupitia kalamu zenu watanzania
wataelewa shughuli nzima ya uhifadhi’,’ alisema Msigwa.
Aidha, shirika linaendelea kutekeleza sera ya ujirani mwema
ambapo pamoja na kutoa elimu ya uhifadhi shirika litaendelea kutekeleza miradi
ya ujirani mwema iliyoanzishwa na jamii kwa kuchangia kiasi cha shilingi
bilioni 2.3 kwenye miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/2024, katika
wilaya 20 za kipaombele.
Na. Zainabu Ally - Dododma
0 Maoni