WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaasa Watanzania watambue kuwa utulivu, amani, umoja na mshikamano ndiyo nguzo muhimu katika ustawi wa Taifa kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Julai 23, 2023) wakati
akizungumza na washiriki wa Kongamano la Mafunzo ya Shirikisho la Kimataifa la
Polisi Wanawake (IAWP) Kanda ya Afrika lililofanyika kwenye uwanja wa Uhuru,
jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu ambaye amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwenye ufunguzi wa kongamano hilo, amesema: “Uhuru huu wa mawazo
tulionao hapa nchini unatolewa kikatiba. Na pia uhuru tulionao unaenda na
wajibu. Watu wasisahau kuwa umoja wa nchi umejengwa siku nyingi. Kwa hiyo
tusitamani kuuharibu kwa manufaa ya watu wachache,” amesisitiza.
Amewataka washiriki wa kongamano hilo, wakawe chachu ya
mabadiliko katika utendaji kazi na wawe mfano kupitia maarifa mapya
watakayoyapata. “Nendeni mkawashirikishe wenzenu ambao hawajapata fursa ya
kushiriki katika mafunzo haya ili wote kwa pamoja mpate manufaa ya Tanzania
kuwa mwenyeji wa kongamno hili la mafunzo.”
Kuhusu umuhimu wa mafunzo, Waziri Mkuu amesema: “Askari wa
kike, changamkieni fursa za mafunzo ya taaluma adimu ndani ya Jeshi la Polisi,
na hii ni namna bora ya kuongeza uwakilishi wa wanawake katika kila idara ndani
ya jeshi.”
Katika kongamano hilo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
alitunukiwa tuzo maalum kwa kutambua na kuthamini mchango wa askari wa kike
nchini na kuwaamini kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki
hao, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni amesema Tanzania iko
salama chini ya usimamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF
Net), Kamishna wa Utawala na Rasilmali Watu wa Jeshi Polisi, Suzan Kaganda
alisema mtandao huo ulianzishwa Oktoba, 2007 ili kuongeza ubunifu miongoni mwa
wanachama wake na kuongeza tija ya utoaji huduma kwa jamii.
“Kupitia mtandao huu, madawati 420 yameanzishwa kwenye vituo
vya polisi kote nchini ambapo tumeweza pia kuanzisha madawati 79 ya kisasa
kupitia kwa wadau. Madawati hayo yametumika kutoa elimu na kuwezesha kuzuia
makosa ya unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.”
Amesema siku hizi watu wanatoa taarifa za mara kwa mara
ikilinganishwa na hapo zamani na kwamba wanatoa huduma kwa watoto na wanaume.
‘Wanaume wasisite kutayumia madawati hayo pindi wanapopata changamoto,”
amesisistiza.
Chanzo: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni