Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (MB)
ameelekeza watumishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA)
kuzitangaza kimkakati Hifadhi za Taifa ambazo bado hazijaweza kujitegemea
kimapato, zijitegemee ili ziweze kuchangia katika pato la Taifa.
Ameyasema hayo leo tarehe 11.07.2023 alipotembelea Banda la
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya
Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Kurasini jijini Dar es Salaam,katika
maelezo yake alizitaja hifadhi hizo kuwa ni Burigi-Chato, Rumanyika- Karagwe,
Kitulo, Katavi na Ibanda - Kyerwa.
Aidha, Mhe.Masanja
amewataka TANAPA kushirikiana na Mawakala wa Utalii nchini kuandaa safari za
kutembelea hifadhi hizo kwa gharama nafuu ili kukuza utalii wa ndani. Alitolea
mfano kuwa uhamasishaji huo pia, ujikite katika taasisi za Serikali na zisizo
za kiserikali, wageni wakaazi na wasio wakaazi “expatriates” walioko katika
maeneo ya migodi kama Geita na kwingineko.
"Ili kuongeza idadi ya watalii watakao tembelea hifadhi
zetu niwaelekeze TANAPA kukaa na wadau na kuangalia njia bora za kukuza utalii
wa ndani na kupanua wigo wa kutangaza utalii wa ndani kwa ajili ya kulifikia soko kubwa zaidi, pia
shirikianeni na vijana wenye taaluma za
uhifadhi na utalii wazijue fursa za uwekezaji zilizopo katika hifadhi za taifa
wawekeze na kunufaika nazo,” aliongeza Mhe. Masanja.
Hata hivyo, aliwataka wadau wa utalii kushirikiana na taasisi
zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa vifurushi vya bei nafuu
kwa nyakati za Maonesho na sikukuu kuvutia wananchi wengi zaidi kutembelea
vivutio hivi adimu.
Maonesho hayo ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini
Dar es Salaam yalianza takribani siku 11 zilizopita na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 13.07.2023.
Na. Jacob Kasiri - Dar es Salaam.
0 Maoni