WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na Kamati ya Usalama ya Mkoa huo wafanye uchunguzi zaidi na kwa haraka kuhusiana na tukio la kupotea kwa binti Esther Noah Mwanyiru ambaye alikuwa akisoma shule ya sekondari ya Panda Hill mkoani humo.
Waziri Mkuu
ametoa agizo hilo jana, baada ya kupokea clip yenye maelezo ya mzazi wa binti
huyo ambaye alikuwa akisoma kidato cha tano, tahsusi ya PCB kwenye shule hiyo.
Katika clip
hiyo, Mama yake Esther anadai kwamba yeye na mume wake waliitwa na uongozi wa
shule hiyo na kujulishwa kwamba Esther hajaonekana tangu asubuhi ya tarehe 18
Mei, 2023 na kwamba hadi sasa zimepita siku zaidi ya 20 wamekuwa wakimtafuta
binti yao kila mahali lakini hakuna dalili za kumpata.
Mama Esther
anadai kuwa Esther aliacha ujumbe wa maandishi akiwaaga rafiki zake na kuomba
Mwalimu Jimmy aache kuwafanyia wanafunzi wengine kitendo alichomfayia yeye
kwani kimesababisha maisha yake kuwa magumu.
“Naomba
umfikishie salamu Mwalimu Jimmy, mwambie ameyafanya maisha yangu kuwa magumu
sana hapa shuleni. Asiendelee kuwafanyia wanafunzi wengine kama alivyoyafanya
maisha yangu mimi kuwa magumu,” alisema mama yake Esther akisoma sehemu ya
ujumbe huo.
CHANZO: Ofisi
ya Waziri Mkuu
0 Maoni