Watoto wa Uganda Ghetto Kids watinga fainali ya British Got Talent

 

Kundi la madansa watoto wanaotoka katika mazingira magumu nchini Uganda, linakaribia kuweka historia, baada ya kutinga fainali ya kipindi cha vipaji cha Uingereza cha British Got Talent.

Watoto hao wamekuwa wakiwavutia mno majaji pamoja na mashabiki Uingereza kwa aina ya unenguaji wao na miondoko yao ya kusakata muziki.

Kundi hilo la Ghetto Kids limekuwa kundi la kwanza kuminyiwa “golden buzzer” (kitufe cha dhahabu) na moja wa majaji, hata kabla hawajamaliza shoo.

Kundi ama mtu anayepata kuminyiwa “golden buzzer” hupata nafasi ya kuingia moja kwa moja hatua ya nusu fainali, hivyo Ghetto Kids wakatinga hatua hiyo.

Kwa kupata kura nyingi za umma kundi la Ghetto Kids sasa ni miongoni mwa washiriki 10 ambao watashiriki katika fainali ya British Got Talent, Jumapili.

Kundi hiyo linaundwa na watoto sita ambao wanaumri wa kuanzia miaka mitano hadi 13 kutoka katika familia masikini katika Jiji la Kampala, linalelewa na Dauda Kavuma ambaye ni meneja wao.

Chapisha Maoni

0 Maoni