Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamedi Janabi, amewashauri wataalamu wa afya kuweka msisitizo katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya zao ili waweze kujua hali zao na kuanza kupata matibabu mapema na kuepuka madhara zaidi.
Prof. Janabi
ameyasema hayo wakati wa kongamano la kitaaluma lililofanyika leo na
kuhudhuriwa na Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka HeathCare Global (HCG) Cancer
Center ya Ahmedabad -India, kongamano hilo limelenga kubadilishana uzoefu wa
matibabu ya saratani ya matiti baina ya kituo hicho na MNH-Mloganzila.
Prof. Janabi
ameongeza kuwa uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Upanga na Mloganzila hivi
karibuni utaeandesha zoezi maalumu la kufanya uchunguzi wa afya za watumishi
wake ambapo utafanya uchunguzi wa saratani ya matiti na saratani ya shingo ya
kizazi wa wanawake na saratani ya tezi dume kwa wanaume.
“Tumeamua
kufanya uchunguzi wa afya za watumishi kwakuwa mara nyingi tumekuwa tukiweka
kipaumbele katika kuchunguza afya za jamii na sisi kujisahau, umuhimu wa
uchunguzi huu wa hiyari kwa watumishi ni kubaini kama mtu ana maradhi haya ili
aweze kuanza matibabu mapema na kuepuka madhara zaidi” amebainisha Prof.
Janabi.
Prof. Janabi
amesisitiza wataalamu kuendelea kumhudumia mgonjwa kwa pamoja (teamwork) ili
kuweza kushauriana na kutoa matibabu stahiki na kwa wakati badala ya kila
mtaalamu kumuona mgonjwa kwa wakati wake.
Kwa upande
wake Daktari Bingwa kutoka HGC Cancer Center ya India, Dkt. Tanay Shah amesema
matibabu ya saratani duniani yanaendana na mabadiliko ya teknolojia hivyo ili
kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja ni vyema kuendelea kujifunza na
kubadilishana uzoefu miongoni mwa wadau wa sekta ya afya.
Ameongeza
kuwa hospitali yao imekuwa ikishirikiana na hospitali mbalimbali nchini kwa
kuleta madataktari na wataalamu wengine wa afya kuja kufanya kazi katika
hospitali hizo kwa lengo la kubadilishana uzoefu na ujuzi walionao.
Naye, Daktari
Bingwa wa Upasuaji MNH-Mloganzila, Dkt. David Antanamsu amefafanua kuwa
saratani ya matiti ni saratani ya pili Duniani kwakuwa inaongoza kwa asilimia
15 ya saratani zote zinazowakumba wakina mama.
Ameongeza
kuwa matibabu ya saratani ya matiti kwa wakina mama ikihusisha kurekebisha titi
bila kuliondoa inafanyika MNH-Mloganzila na kuwasihi wenye changamoto hizo
kufika kwa matibabu.
0 Maoni