Waziri wa
Fedha Na uchumi Dk Mwigulu Lameck Nchemba amewasilisha Bajeti Kuu ya Serikali
kwa mwaka mwaka wa fedha 2023/24 inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni
44.39 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika.
Akiwasilisha
bajeti hiyo leo katika Bunge la 12, mkutano wa 11 kiako cha 49 Dk. Nchemba amesema
kwamba jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 31.38, sawa
na asilimia 70.7 ya bajeti yote.
Ameongeza
kwamba kwamba kati ya mapato hayo, mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 26.73 na mapato yasiyo ya kodi
(Wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa) yanakadiriwa kuwa shilingi
trilioni 4.66.
Amesema misaada
na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa
Maendeleo inatarajiwa kuwa shilingi trilioni 5.47, ambapo pia Serikali
inatarajia kukopa shilingi trilioni 5.44 kutoka soko la ndani ambapo shilingi
trilioni 3.54 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali
zinazoiva na kiasi cha shilingi trilioni 1.90 ni kwa ajili ya kugharamia miradi
ya maendeleo.
Vilevile,
Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 2.10 kutoka soko la nje kwa
masharti ya kibiashara kwa lengo la kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Dk. Nchemba
amesema katika mwakawa fedha 2023/24, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi
trilioni 44.39 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.
Ameongeza
kuwa kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 30.31 zimetengwa kwa ajili ya
matumizi ya kawaida, ikijumuisha: shilingi trilioni 12.77 kwa ajili ya ulipaji
wa deni la Serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu; shilingi trilioni 10.88 kwa
ajili ya mishahara ikiwemo nyongeza ya mshahara, upandishaji wa madaraja na
ajira mpya.
Pia shilingi
trilioni 1.14 ni ruzuku ya maendeleo kwa ajili ya kugharamia elimumsingi na
sekondari bila ada pamoja na mikopo ya wanafunzi elimu ya juu; shilingi
trilioni 5.52 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC).
Aidha, Dk. Nchemba amesema matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 14.08. Kiasi hicho kinajumuisha gharama za utekelezaji wa miradi mbalimbali katika ngazi ya Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
0 Maoni