Deni la Taifa, mfumuko wa bei vyapaa

 

Serikali imesema kuwa mpaka Aprili mwaka huu, deni lake limefikia Sh79.1 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 13.9 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022.


Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba wakati wa uwasilishaji wa Hali ya Uchumi kwa mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2023/24 kati ya deni hilo, la nje ni Sh51.16 trilioni huku lile la ndani ni Sh27.93 trilioni.


Waziri Mwigulu Nchemba amesaema ongezelo hilo lilitokana na kuongezeka kwa mahitaji ya fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme, elimu na afya.


Aidha, Dk. Nchemba amesema hadi kufikia Machi 2023, Serikali ilikuwa imekopa Sh1.3 trilioni kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo,


MFUMUKO WA BEI 

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba, amesema miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa mfumko wa bei ni kupanda kwa gharama za bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi.

Dk Mwigulu amezitaja bidhaa hizo kuwa ni petroli, mafuta ya kula, mbolea, ngano na malighafi za viwandani huku akisema kwa umuhimu wake katika maisha ya kila siku athari zake ziligusa wengi.


Nyingine  ni kupungua kwa upatikanaji wa mazao ya chakula katika baadhi ya masoko ya ndani kulikosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, hususan katika maeneo yanayotegemea mvua za vuli kwa ajili ya kilimo.

Chapisha Maoni

0 Maoni