Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali haitodharau maoni na ushauri wanaoutoa kuhusu maeneo yenye hofu kwenye mradi wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Pia,
Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuwa na imani na Serikali
pamoja na wawakilishi wao ndani ya Bunge, kwani Serikali imejidhatiti
kuhakikisha bandari inakuwa na ufanisi unaoendana na mahitaji ya sasa na kwa
kuzingatia manufaa ya kijiografia ya nchi yetu.
Waziri Mkuu
ameyasema hayo leo (Jumanne, Juni 20, 2023) katika sherehe za Maadhimisho ya
Miaka 40 ya chuo cha International Evangelism Centre kilichoko Sakila jijini
Arusha. Amesisitiza kwamba bandari haijauzwa, bali Serikali inataka kubadilisha
muwekezaji ili iweze kuendeshwa kwa ufanisi na tija zaidi.
Amesema
pamoja na maboresho yaliyofanyika, hali ya utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam
imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani
kikanda. Kwa mfano, wastani wa meli kusubiri nangani kwa Bandari ya Dar es
salaam ni siku tano ikilinganishwa na wastani siku moja na nusu kwa Bandari za
Mombasa na Durban.
Amesema
udhaifu huo uliopo katika bandari hiyo unasababisha meli kusubiri muda mrefu
nangani na hivyo kuongeza gharama, kwa
siku moja ni takriban Dola za Marekani 25,000, sawa na takriban shilingi
milioni 58 kwa siku.
Waziri Mkuu
amesema kitendo cha meli kutumia muda mrefu kupakia na kupakua shehena gatini
kwa wastani wa siku tano ikilinganishwa na siku moja inayokubalika kimataifa
kinasababisha meli kubwa kutokuja katika bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa
Majaliwa amesema hali hiyo huikosesha nchi mapato ambayo yangeweza kutumika
katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini ambayo ingesaidia
kukuza uchumi na kuboresha huduma za wananchi.
Waziri Mkuu
amesema ili kutatua changamoto za bandari zilizopo na kuongeza ufanisi katika
mapato, ajira na kuchagiza sekta nyingine za kiuchumi, Serikali ilifanya
maamuzi ya kutafuta wawekezaji wapya wanao endana na dhima ya Serikali.
Amesema
tarehe 10, Juni, 2023 Bunge liliridhia mkataba unaohusu makubaliano ya
mahusiano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai (IGA) ili
kuwezesha majadiliano ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Amesema
miradi hiyo ni pamoja na ya uendelezaji na uboreshaji wa huduma za bandari
nchini. “Kilichofanyika sasa ni kuwezesha tu baadaye kuwa na mikataba ya maeneo
maalum ambayo itazingatia maslahi ya nchi kisheria na kibiashara bila kuathiri
usalama Taifa.”
Pia,
Mheshimiwa Majaliwa amesema wakati wa kuingia mikataba utakapofika wataalamu wa
uchumi nchini wataishauri Serikali kuhusu muda wa uendeshaji wa uwekezaji huo,
hivyo amewataka wananchi waendelee kuwa na subra.
CHANZO: Ofisi
ya Waziri Mkuu
0 Maoni