BOT: Upungufu wa dola upo ila bado ni himilivu

 

Benki Kuu ya Tanzania (BOT), imekiri kuwapo kwa upungufu wa fedha za kigeni hususan dola ya Marekani na kuwatoa hofu wananchi kuwa, upungufu huo ni himilivu kwa kuwa nchi bado ina akiba ya kutosha.

Mkurugenzi wa Tafiti na Sera za Uchumi Dk. Suleiman Misango ametoa kauli hiyo leo Dar es Salaam, wakati akielezea Mwenendo wa Uchumi na Fedha za Kigeni nchini, katika mkutano wake na Wahariri wa Vyombo vya Habari.

Dk. Misango amesema kwamba akiba ya fedha za kigeni ni ya kuridhisha, nchi ina Dola za Marekani bilioni 4.9 kwa mwezi Mei 2023, ambazo zinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa zaidi ya miezi mine.

"Wananchi hawana sababu ya kuwa na hofu ya upungufu wa fedha za kigeni, kama nchi tunauwezo mzuri na kila mwezi BOT inauza dola milioni 2 kila siku ili kukabiliana na upungufu uliojitokeza katika soko la fedha za kigeni," alisema Dk. Misango.

Hata hivyo Dk. Misango amesema kuwa upungufu huo wa dola nchini unatarajiwa kupungua zaidi katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Septemba kutokana na kuanzia kwa msimu wa utalii na kuanza kwa uuzaji nje wa mazao ya biashara.

Aidha, Dk. Misango amesema kuanzia mwaka 2022 hadi hivi sasa, mwenendo wa uchumi wa dunia umekuwa sio wa kuridhisha kutokana na sababu za Uviko-19, Vita ya Ukraine na Urusi pamoja na Mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kuwa pamoja na changamoto hizo zilizoziathiri nchi zinazoendelea pamoja na nchi zilizoendelea, uchumi wa Tanzania bado unafanya vizuri ukilinganisha na nchi zingine za Afrika zinazolingana nayo kiuchumi.

Akielezea sababu zingine zilizochangia upungufu wa dola nchini, Dk. Misango amesema kuwa ni uamuzi wa Benki Kuu duniani kufanya uamuzi kubadilisha mwelekeo wa sera ya fedha kwa kupandisha riba.

Dk. Misngo ametoa mfano wa Benki Kuu ya Marekani wa kupandisha riba kutoka asilimia 0.75 hadi kufikia asilimia 5.52, ikiwa ni sawa na ongezeko la riba la asilimia 500.

"Ongezeko la riba la Marekani limepelekea uwapo wa upungufu wa dola kutokana watu sasa kuvutiwa kupeleka dola zao Marekani kwa kuwa kunafaida kubwa na hata kuathiri uwekezaji na mikopo nafuu kwa nchi zinazoendelea," alisema Dk. Misango.

Pamoja na mambo mengine Dk. Misango alielezea kwa kina hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Benki Kuu katika kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni pamoja na mikakati iliyochukuliwa Serilali katika kukabiliana na hali hiyo.


Chapisha Maoni

0 Maoni