Kambi ya wanajeshi wa Uganda yashambuliwa Somalia

 

Jeshi la Uganda linachunguza shambulizi lililofanywa kwenye kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) ya vikosi vya Umoja wa Afrika katika mji wa Bulo nchini Somalia Ijumaa asubuhi.

Msemaji wa UPDF felix Kulayigye ameiambia Nation.Africa kwamba shambulizi hilo limetekelezwa na waasi wa kigeni, bila ya kutoa taarifa zaidi.

Amesema kwamba anawasiliana kwanza na Makao Makuu ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS), ndipo atakapotoa taarifa rasmi.

Washambuliaji hao wanaohisiwa kuwa ni wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab, walijaribu kuvamia kambi hiyo iliyopo kilomita 120 kusini mwa Jiji la Mogadishu ambapo milipuko kadhaa ilitokea.

Hakuna taarifa zozote za kuwapo kwa majeruhi ama vifo, lakini vyanzo vinasema kwamba kambi hiyo ya mji wa Bulo inawanajeshi wengi wa ATMIS.

Chapisha Maoni

0 Maoni