Clatous Chama apigwa nondo mechi tatu

 

Kiungo machachari  wa Simba raia wa Zambia, Clatous Chama, maarufu kama mwamba wa Lusaka amefungiwa michezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kutozwa faini ya Shilingi 500,000.


Uamuzi huo umetolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kutokana na kumkanyaga makusudi mchezaji Abal Kassim wa Ruvu Shooting wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara hivi karibuni, tukio lililotokea wakati wachezaji hao hawagombei mpira, jambo lililosababisha mwamuzi wa michezo ashindwe kuona.



Kutokana na uamuzi huo, Chama sasa atakosa michezo miwili iliyobaki ya kumaliza msimu, ambayo timu yake itacheza.


Adhabu hiyo ni kwa kuzingatia Kanuni ya 41:5 (5:2) ya ligi kuu kuhusu udhibiti wa wachezaji.


TPLB pia imemfungia kiongozi wa African Lyon ya Dar es Salaam Salehe Hassan maarufu kama Mkele kwa miezi 6 na kutozwa faini ya sh 500,000 kwa kosa la kumtolea lugha za kejeli na matusi Kamishna wa michezo .

Chapisha Maoni

0 Maoni