Baba mzazi wa Marehemu Joel Misesemo aliyejirusha katika jengo la ghorofa la Derm Plaza lililopo Makumbusho, ameeleza mapito ya mwanaye kabla ya umauti.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu maziko ya mtoto wake baba mzazi wa marehemu, Mzee Mattson Misesemo amesema marehemu Joel alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi kwa muda mfupi lakini alipata matibabu na kuendelea na shughuli zake kama kawaida.
Akizungumza kwa uchungu Mzee Mattson amesema Joel hakuwahi kumtaarifu kuwa na changamoto yeyote kuhusu maisha yake kwani alikuwa anaishi na familia yake na kudai hajui kilimpata nini hadi akaamua kujirusha ghorofani.
Jeshi la polisi
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro alithibitisha kifo cha Joel Misesemo aliyejirusha ghorofani Makumbusho.
Majirani wafunguka
Baadhi ya majirani waliomzungumzia wamesema Joel alikuwa ni mtu wa watu, alijichanganya na kuongea na kila mtu mtaani na kuwa marehemu enzi za uhai wake katika ghorofa ambayo umauti ulimkuta alikuwa akienda kufanya mazoezi kipindi alivyokuwa mgonjwa.
Janeth Andendekise, ni binti aliyelelewa na marehemu tangu mwaka 2016 amesema baada ya wazazi wake kufariki alipitia changamoto mbalimbali za kimaisha ikiwemo kuumwa lakini alipokutana na Joel alimpokea na kukubali kuishi naye mpaka alipoweza kuanza maisha ya kujitegemea.
Janeth anasema mara ya mwisho kuzungumza na marehemu ilikuwa Jumatatu akiwa visiwani Zanzibar anapofanya shughuli zake za biashara na kumtaarifu kuwa amepata mchumba na yupo mbioni kwenda kumtambulisha.
Anasema hukuwa anafahamu kama marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kupooza mpaka mke wa marehemu ambaye anamwita bibi alipomueleza kuwa alipooza kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Kuzikwa Kinondoni
Mwili wa marehemu Joel unatarajiwa kuzikwa Ijumaa katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Marehemu Joel enzi za uhai wake alikuwa ni mshehereshaji na mhamasishaji alikuwa na mke hakuwahi kufanikiwa kuwa na mtoto lakini aliwalea watoto wa watu wengine wanne waliopitia matatizo mbalimbali.
Chanzo:Mwananchi/globaltv/tanpoltz
0 Maoni