Waziri Mkuu wa Japan Kishida atupiwa bomu

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida ameondolewa bila madhara kutoka katika eneo la hafla ya umma, baada ya kubainika kurushwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu la moshi likimlenga yeye.

Chombo kimoja nchini humo kimeripoti kuwa mtu mmoja mwanaume anashikiliwa kwa kuhusika na tukio hilo, lililotokea eneo la Wakayama, ambapo Bw. Kishida alitarajiwa kutoa hotuba yake.

Mashahidi wamesema walimuona mtu akirusha kitu, na kufuatiwa na moshi huku wengine wakisema walisikia kishindo kikubwa. Hakuna taarifa za kuwapo majeruhi.

Shirika la Utangazaji la Japan NHK, limemnukuu Waziri Mkuu Kishida akisema kwamba “kulikuwa na mlipuko mkubwa katika eneo la hafla”.

Polisi Japan wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, lakini pia wanatarajia kuomba radhi kwa kuwatia hofu watu wengi na kusababisha usumbufu.

Imeelezwa kuwa watu walianza kutimka mbio na kuibuka hali ya taharuki, baada ya mtu mmoja kusikika akisema kuna bomu limetupwa.

Chanzo: BBC

Chapisha Maoni

0 Maoni