Ujenzi barabara ya lami ya Chanika–Kilole kuchochea fursa za maendeleo mji wa Handeni

‎Wananchi wa kata za Chanika na Kwenjugo Halmashauri ya Mji wa Handeni mkoani Tanga wanatarajia kunufaika na huduma za kijamii na fursa za kiuchumi kufuatia ujenzi wa barabara ya Chanika–Kilole yenye urefu wa kilomita 1.7 inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 1.2.‎

‎Ujenzi wa barabara hiyo unaotekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia vyanzo viwili vya fedha ambavyo ni Fedha za Tozo na Mfuko wa Jimbo unalenga kuboresha mawasiliano kati ya kata hizo na kurahisisha shughuli za kila siku za wananchi.‎

‎Akielezea utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa TARURA wilaya ya Handeni Lusubilo William amesema kuwa kati ya fedha hizo shilingi milioni 755 zilizotokana na Fedha za Tozo zimewezesha ujenzi wa kilomita 1.1 huku shilingi milioni 475 kutoka Mfuko wa Jimbo zikitumika kujenga mita 600 za barabara hiyo.‎

‎Amesema kuwa pamoja na ujenzi wa barabara, mradi umehusisha pia ujenzi wa boksi kalavati na mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 1.6 ambapo kwa sasa kazi zinazoendelea ni ujenzi wa mitaro katika pande zote mbili za barabara ili kuhakikisha maji yanapita vizuri na kulinda uimara wa miundombinu hiyo.‎

‎Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Chanika Mhe. Habib Mbota amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha zilizofanikisha ujenzi wa barabara hiyo akieleza kuwa hapo awali hali ya barabara ilikuwa mbaya na kusababisha changamoto kwa wananchi ikiwemo ajali zilizohusisha watoto kutokana na kutokuwepo kwa kivuko salama.‎

‎Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa mkombozi kwa wakazi wa maeneo hayo kwani sasa wataweza kufika katika zahanati na maeneo mengine muhimu kwa urahisi zaidi bila kukabiliwa na vikwazo vilivyokuwepo awali.‎

‎Ameongeza kuwa ni wajibu wa wananchi kushirikiana na serikali kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.‎

‎Naye, mkazi wa mtaa wa Chang'ombe Bi. Amina Hussein amesema kuwa mvua zilipokuwa zikinyesha ilikuwa vigumu kwa wananchi kuvuka barabara hiyo hali iliyowaathiri zaidi wanawake watoto na wagonjwa waliokuwa wakihitaji kufika katika zahanati na shule.‎

‎Amesema ujenzi wa barabara hiyo umerejesha matumaini kwa wananchi wa eneo hilo kwani utakapokamilika utarahisisha usafiri na kuwawezesha kupata huduma muhimu kwa wakati bila vikwazo vya hali ya hewa.‎

‎Naye, Mwenyekiti wa mtaa wa Chang'ombe, Bw. Juma Kingo amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua fursa mpya za kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuwa kutarahisisha kwa usafiri na usafirishaji wa bidhaa na kuchochea ukuaji wa biashara na kuongeza shughuli za kiuchumi.



Chapisha Maoni

0 Maoni