Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha wananchi wanapata makaazi bora, salama na yanayokidhi mahitaji ya maisha ya sasa na yajayo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 08 Novemba 2026, katika hafla ya uzinduzi wa mauzo ya nyumba za kisasa za mradi wa Saateni, iliyofanyika Hoteli ya Golden Tulip,Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025–2030 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi, kuimarisha ustawi wa jamii na kupanua fursa za umiliki wa nyumba.
Rais Dkt. Mwinyi amesema sekta ya makaazi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo Serikali itaendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha watumishi wa umma, vijana, wafanyabiashara pamoja na wananchi wa kipato cha chini na cha kati kumiliki nyumba kwa masharti nafuu.
Ameelekeza Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) kuendelea kubuni mifumo rafiki ya malipo na kuimarisha ushirikiano na taasisi za fedha ili kupanua fursa za umiliki wa nyumba, akisisitiza kuwa makaazi bora hayapaswi kuwa fursa ya wananchi wenye uwezo mkubwa wa kifedha pekee.
Vilevile, amelitaka Shirika hilo kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi inayoendelea na kuanzisha mingine mipya, huku akiwahimiza wananchi wanaonunua nyumba kutimiza masharti ya manunuzi na kufanya malipo kwa wakati ili fedha hizo ziendelee kutumika kutekeleza miradi mingine ya makaazi.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi amelitaka Shirika la Nyumba Zanzibar kuzingatia maslahi ya familia zilizopisha eneo kwa ajili ya mradi wa Saateni kwa kuwatengea nyumba maalum na kuwapatia punguzo la asilimia 50 ya kodi, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kufanikisha mradi huo.
Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuboresha makaazi katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, yakiwemo Michenzani, Kilimani na maeneo mengine yenye nyumba zilizochakaa, pamoja na kuendeleza ukarabati wa nyumba za Mji Mkongwe.
Pia amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango miji na miradi ya maendeleo inayolenga kujenga makaazi ya kisasa yenye mazingira bora na huduma muhimu.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi pamoja na Shirika la Nyumba Zanzibar kwa juhudi za kuimarisha sekta hiyo kupitia miradi ya Kisakasaka, Chumbuni, Kiembe Samaki, Mombasa na Saateni.
Wakati wa hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ameshuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano baina ya Shirika la Nyumba Zanzibar na taasisi mbalimbali, zikiwemo ZURA na ZIC.
Naye, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Mhe. Rahma Kassim Ali, amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa juhudi za kuimarisha sekta ya makaazi na kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kuishi katika nyumba bora na salama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Sultan Said Suleiman, amesema mradi wa Saateni unatarajiwa kuwa na nyumba 209, pamoja na maeneo ya biashara, huduma za kijamii na maegesho ya magari.
Amesema utekelezaji wa mradi huo umehusisha ushirikiano wa wananchi, ambapo familia 25 zimepisha eneo kwa ajili ya ujenzi na zimetengewa nyumba kama sehemu ya kutambua mchango wao katika kufanikisha mradi huo.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Serikali, Shirika la Nyumba Zanzibar, taasisi za fedha pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya makaazi.


0 Maoni