Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Malima, kuwachukulia hatua wote wanaohusika kuchochea migogoro ya wakulima na wafugaji bila kujali vyeo vyao, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwajibika katika kulinda usalama wa wananchi na kutatua matatizo yao.
Ameyasema hayo akihitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Lindi kwa kuzungumza na wananchi wa Somanga, Jimbo la Kilwa Kaskazini, ambako amepokea hoja kuhusu migogoro ya ardhi, huduma za afya, barabara na mahitaji ya wakulima.
Makamu wa Rais amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua, huku akitaka viongozi na watendaji wa vijiji na vitongoji wapimwe kwa namna wanavyoshughulikia migogoro na matatizo ya wananchi. Amesisitiza kuwa yeyote atakayebainika kuchochea migogoro hiyo achukuliwe hatua bila kusita.
Makamu wa Rais amewahimiza wananchi kutunza na kuenzi uwekezaji wa Serikali unaoendelea mikoa ya Kusini ili itoe manufaa yaliyokusudiwa. Amesisitiza umuhimu wa viongozi kushughulikia matatizo ya wananchi, huku wananchi wakilinda miundombinu inayowezesha maendeleo katika maeneo yao.
Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Mhe. Kinjeketile Ngombale Mwiru, amedai kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji imesababisha baadhi ya wananchi kupigwa na wengine kuachwa na ulemavu. Ameiomba Serikali kuharakisha hatua za kukomesha hali hiyo ili wananchi waendelee na shughuli zao kwa usalama.
Katika afya, Ngombale Mwiru ameomba kujengwa kwa hospitali yenye hadhi ya wilaya katika Jimbo la Kilwa Kaskazini, akieleza kuwa baadhi ya wananchi hulazimika kusafiri takribani kilometa 180 kwenda Kivinje kutafuta matibabu. Amesema umbali huo unawaweka wagonjwa na wajawazito katika mazingira magumu, huku baadhi wakijifungulia njiani.
Mbunge huyo pia ameomba fedha za ziada kwa ajili ya kuboresha barabara za ndani na kuimarisha njia zinazounganisha jimbo hilo na Rufiji. Pamoja na kupongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji katika maji na kilimo, ameomba mbolea za ruzuku ziwafikie wakulima mapema na kuongezwa kwa matrekta ili kupanua uzalishaji.
Makamu wa Rais, amehitimisha ziara hiyo Lindi kuanza ziara Mkoa wa Pwani.

0 Maoni