Dkt. Mwigulu aagiza TAKUKURU kuchunguza miradi Shinyanga

WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga kuchunguza miradi iliyolalamikiwa kuchelewa na kujengwa chini ya kiwango, akitaka apewe moja kwa moja taarifa ili hatua zichukuliwe.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Novemba 9, 2026), katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya JASCO, Kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga, baada ya kupokea malalamiko kuhusu utekelezaji wa miradi ya barabara, stendi na soko.

“Hebu tusaidie kuangalia maeneo haya ambayo yamelalamikiwa. Na hiyo taarifa niipate mwenyewe ili niweze kuchukua hatua haraka,” amesema akimwelekeza Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga.

Amesema Serikali haitavumilia wananchi kukosa manufaa ya miradi ambayo tayari imepelekewa fedha.

“Tutachukua hatua kali tukibaini kuna ubadhirifu wowote ama kuna uzembe umefanyika katika eneo lolote lile,” amesema.

Awali, Mbunge wa Shinyanga Mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amelalamikia kasi ya ujenzi wa stendi na barabara ya kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kupitia mradi wa TACTIC.

Katambi amehoji pia ubora wa ujenzi wa barabara ya Old Shinyanga–Bubiki, akisema baadhi ya sehemu zinaharibika kabla ya kazi kukamilika.

Kuhusu soko kuu, ameomba Serikali Kuu iongeze fedha ili kukamilisha ujenzi wake, akieleza kuwa manispaa imekuwa ikitumia mapato yake ya ndani kutekeleza mradi huo.

Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu amesema ukaguzi utabaini kinachoendelea katika miradi iliyolalamikiwa na kuwezesha Serikali kuchukua hatua zinazostahili.

Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa viongozi na watendaji katika ngazi zote wanapaswa kutimiza wajibu wao ili wananchi wanufaike na fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo.

Chapisha Maoni

0 Maoni