Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala, ametoa onyo kali dhidi ya uharibifu wa vyanzo vya maji baada ya kubaini uchimbaji haramu wa madini ndani ya Mto Mvuha, katika Kijiji cha Bungu.
Chanzo hicho muhimu cha maji kimekumbwa na uharibifu mkubwa unaotokana na shughuli za uchimbaji ndani ya mto, hali inayotishia usalama na ubora wa maji kwa wananchi na viumbe hai wanaoutegemea.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, ikiongozwa na Mhe. Kilakala, ilifanya ziara ya kushtukiza katika eneo hilo ambapo ilibaini uwepo wa uchimbaji ndani ya eneo la hifadhi ya mita 60 kutoka kingo za mto, kinyume na Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji, Sura ya 331, Toleo la Marekebisho la mwaka 2023.
Akizungumza mara baada ya kukagua uharibifu huo, Mhe. Kilakala alionyesha kusikitishwa na hali aliyoikuta na kutoa maelekezo ya haraka.
"Kutokana na uharibifu huu, Jeshi la Polisi linatakiwa kumshikilia mara moja mtuhumiwa Bw. Omari Muhondogwa kwa hatua za kisheria. Pia, Tume ya Madini isitishe leseni yake mara moja," alisema DC Kilakala.
Aidha, DC Kilakala ametoa siku saba kwa Bw. Muhondogwa kuhakikisha anarejesha mto katika hali na mwelekeo wake wa asili, huku akiwaamuru wananchi wote waliopo eneo la hifadhi kuondoka mara moja kupisha zoezi la urejeshaji.
Kwa mujibu wa kamati hiyo, uchimbaji huo umesababisha kujaa kwa tope mtoni, kuharibika kwa mfumo wa asili wa mtiririko wa maji na kuhatarisha ubora wa maji.
Kamati ya Ulinzi na Usalama imesisitiza kuwa haitamvumilia mtu yeyote anayeharibu vyanzo vya maji na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


0 Maoni