Na. Mwandishi Wetu – St Petersburg, Urusi
ST PETERSBURG. Tanzania inalenga kuongeza tija na thamani ya mazao ya misitu kwa kutumia teknolojia za kisasa za uchakataji, baada ya wataalamu wake kushiriki mafunzo maalumu nchini Urusi.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Septemba 27 hadi Oktoba 4, 2026, jijini St Petersburg, ni sehemu ya utekelezaji wa Hati ya Makubaliano kati ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Chuo Kikuu cha Taifa cha Misitu cha St Petersburg (SPbSFTU) kupitia Programu ya Maendeleo ya Kitaaluma.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Profesa Dos Santos Silayo, Mratibu wa programu hiyo upande wa Tanzania, Mhifadhi Mkuu Jared Elly Otieno, alisema wataalamu hao wamepata ujuzi wa vitendo kuhusu teknolojia za kuboresha ubora wa mbao, ufuatiliaji wa ukuaji wa misitu, usimamizi wa ikolojia na utunzaji wa takwimu za rasilimali za misitu.
Alisema maarifa hayo yatasaidia kuongeza kiwango cha urejeshaji wa mbao baada ya uvunaji (timber recovery rate) na kuongeza thamani ya mazao ya misitu kupitia uchakataji wa kisasa.
Otieno alisema ujuzi huo pia utatumika kuwaelimisha wadau wa viwanda vya misitu nchini ili kuongeza uzalishaji wa samani na bidhaa nyingine za mbao ndani ya Tanzania na kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje.
Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Dkt. Revocatus Mushumbusi, na ulihusisha wataalamu kutoka TFS, TAFORI, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Ziara hiyo ilihusisha pia kutembelea taasisi na vituo mbalimbali vya misitu, ikiwemo SPbSFTU, Kituo cha Mafunzo na Utafiti cha Lisinsky na vituo vya uchakataji wa mazao ya misitu, kwa lengo la kujifunza mifumo ya matumizi ya teknolojia katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Otieno, ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu, kuongeza tija kwa wadau, kufungua fursa za ajira katika viwanda vya misitu na kuongeza mapato ya Serikali yatokanayo na biashara ya mazao hayo.


0 Maoni