Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu anayeshughulikia masuala ya mipango na usimamizi wa utendaji serikalini Shaaban Ali Othman amesema kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuanza kuingia mikataba ya utendaji kazi na mawaziri wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Hatua hiyo inalenga kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi na kuhakikisha mipango ya Serikali inaleta matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi.
Wakizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Zanzibar, mawaziri hao, Waziri wa wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anaeshughulikia mipango na usimamizi wa utendaji serikalini, Shaaban Ali Othman, na waziri wa Nchi ofisi ya rais ikulu anayeshughulia siasa na uhusiano wa jamii, Masoud Ali Mohammed walieleza majukumu yao na namna wanavyolenga kuimarisha utendaji wa Serikali katika maeneo waliyopewa, ikiwemo mipango na usimamizi wa utendaji serikalini, pamoja na siasa na uhusiano wa jamii.
Waziri Shaaban amesema mawaziri hao wataingia mikataba ya utendaji kazi na makatibu wakuu wa wizara zao, ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa kwa kipindi cha miaka mitano yanatekelezwa kupitia mipango ya kazi ya kila mwaka.
Aidha, Waziri Shaaban amesema hatua za awali za kupitia mikataba hiyo zimekamilika, huku utaratibu huo ukilenga kuweka mfumo wa kupima utendaji wa mawaziri na viongozi wengine kwa kuzingatia malengo na matokeo wanayopaswa kuyafikia, hususan katika miradi ya kimkakati ya maendeleo.
Mheshimiwa Shaaban amesema kuwa utekelezaji wa majukumu ya viongozi utafuatiliwa kila robo mwaka na nusu mwaka, huku tathmini nyingine ikifanyika katika robo ya tatu kabla ya kuandaliwa kwa ripoti ya mwaka mzima itakayowasilishwa kwa mamlaka husika.
Katika hatua nyingine, Mhe ,Shaaban amesema Rais Mwinyi ameamua kuhamishia jukumu la mipango kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kwenda Ofisi ya Rais, Ikulu, ili kuimarisha uratibu na kuhakikisha mipango ya Serikali inaendana na vipaumbele vya maendeleo ya Zanzibar.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Jamii, Masoud Ali Mohammed, amesema uwepo wa mawaziri wawili katika ofisi hiyo unalenga kuimarisha mawasiliano kati ya Rais na wananchi, pamoja na kuongeza ufanisi katika kushughulikia changamoto zinazowakabili.
Amesema mawaziri hao wamepewa majukumu tofauti ili kurahisisha upatikanaji wa huduma, kupokea maoni ya wananchi na kufuatilia changamoto za kisiasa na kijamii zinazohitaji hatua za Serikali.
Mheshimiwa Masoud amesema katika eneo la siasa atashirikiana na vyama mbalimbali vya siasa ili kuweka mazingira yanayowezesha wadau hao kuwasilisha hoja na mitazamo yao, kwa lengo la kuimarisha mawasiliano na kujenga nchi kwa pamoja.
Waziri Masoud, akizungumzia uhusiano wa jamii, amesema atafuatilia changamoto zinazowakabili wananchi, zikiwemo masuala ya dini na fidia, kwa kushirikiana na taasisi za Serikali zinazohusika.
Aidha, amesema kuwa mfumo wa Sema na Rais utaendelea kupokea changamoto nyingine za wananchi, zikiwemo zinazohusu maji, ardhi na huduma mbalimbali, huku utaratibu maalumu wa fidia ukisaidia kurahisisha ufuatiliaji wa malalamiko hayo.

0 Maoni