Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri kuwa karibu na wananchi, kuwasikiliza na kufuatilia kwa vitendo changamoto zinazowakabili ili kuzitafutia ufumbuzi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 05 Oktoba 2026, katika Viwanja vya Ikulu Zanzibar, wakati akiwaapisha Mawaziri na Naibu Mawaziri walioteuliwa kuongoza Wizara mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Hassan Ali Haji .
Amesema kuapishwa kwa viongozi hao kunakamilisha hatua muhimu ya uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kufuatia utekelezaji wa maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha ACT-Wazalendo.
Rais Dkt. Mwinyi amewataka viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, uadilifu na uwajibikaji, huku wakizingatia kiapo walichokula na kuhakikisha mipango na miradi ya Serikali inatekelezwa kwa wakati na kuleta matokeo halisi kwa wananchi.
Aidha, amewataka kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kupambana na uzembe, urasimu usio wa lazima na ubadhirifu, pamoja na kusimamia kwa tija rasilimali za Serikali.
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa viongozi kufanya kazi kwa pamoja bila kujali tofauti za kisiasa, kijamii au kiitikadi, kwa lengo la kuimarisha amani, umoja, mshikamano na maendeleo ya Zanzibar.


0 Maoni