Naibu Waziri wa Maji atoa siku saba kukamilisha mradi wa maji Urambo

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, ametoa siku saba kwa wakandarasi na wasimamizi wa mradi wa maji Urambo mkoani Tabora kuweka kipaumbele katika kukamilisha kazi zilizobaki ili wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama, akisisitiza kuwa hakuna nafasi ya visingizio baada ya Serikali kuwekeza fedha nyingi katika mradi huo.

Amesema mradi huo ni sehemu ya uwekezaji wa takribani shilingi bilioni 143, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo na wakandarasi kwa kazi iliyofanyika.

Aidha, amewataka wahusika kuongeza kasi ya kukamilisha ulazaji wa mabomba ili maji yawafikie wananchi ndani ya muda uliotolewa.

Sambamba na hilo, Mhandisi Kundo amesisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na mvua nyingi zinazotarajiwa, huku akiwataka wananchi kutumia maji kwa uangalifu na kutoa taarifa mapema wanapoona mabomba yanavuja au kupasuka.

Hata hivyo Mhandisi Kundo ameitaka timu ya usimamizi Mradi wa ujenzi wa  Bwawa la kalemela Mkoani Tabora kuhakikisha mkandarasi anarudi eneo la kazi ndani ya siku saba na kuongeza kasi ya utekelezaji.

akieleza kuwa kati ya madai ya shilingi bilioni tano, tayari amelipwa shilingi bilioni 3.5, zikiwemo shilingi milioni 449 zilizolipwa wiki mbili zilizopita, huku madai ya shilingi milioni 445 yakiwa bado.

Amesisitiza kuwa mkandarasi anapaswa kurejea site mara moja ili kazi zilizobaki zikamilike na wananchi wa Urambo waanze kupata huduma ya maji safi na salama kwa wakati.




Chapisha Maoni

0 Maoni