Wasanii kutoka tasnia mbalimbali, wakiwemo wachekeshaji, wanamuziki, wanamichezo na watu wenye ushawishi nchini, wametajwa kuwa nyenzo muhimu katika kukuza, kuimarisha na kuenzi misingi ya Muungano.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, wakati akifungua kikao kati ya ofisi hiyo na wadau hao kilicholenga kujadili mpango wa kutoa elimu kwa umma kuhusu Muungano. Kikao hicho kilifanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 19, 2026.
Alisema wadau hao ni kundi muhimu lenye uwezo wa kujenga ushawishi na kuhamasisha jamii, hivyo ofisi hiyo imekusudia kutumia majukwaa yao kufikisha elimu ya Muungano kwa makundi mbalimbali, yakiwemo ya vijana.
Aliongeza kuwa elimu ya Muungano ni ajenda ya kudumu inayolenga kuitambulisha jamii kwa taifa lake na kuifahamu historia na chimbuko lake, hivyo ushirikishwaji wa wasanii, waigizaji na watengeneza maudhui ni muhimu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Latifa Mohammed Khamis, alisema ushirikishwaji wa wasanii, waigizaji na watengeneza maudhui ni miongoni mwa mikakati iliyoandaliwa na ofisi hiyo kuhakikisha elimu ya Muungano inawafikia wananchi.
Alisema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, asilimia 77.3 ya Watanzania wamezaliwa baada ya Muungano, hivyo ni muhimu kuweka mikakati ya kutoa elimu kuhusu Muungano kwa kundi hilo.
Kikao hicho cha siku moja kiliwashirikisha wasanii na waigizaji mbalimbali, wakiwemo wachekeshaji maarufu mtandaoni Victor Victor, maarufu Nanga; Mohamed Mwinchande, maarufu Matofali; Ester Luckson, maarufu Mama Chanja; na Amani Nzala, maarufu Nzala.
Wengine ni mtengeneza maudhui mtandaoni Vicent Njau, maarufu Kiredio; mwandishi wa habari na mjasiriamali Fredrick Bundala, maarufu Sky Walker; pamoja na John Rojas, maarufu Simple the Boy.


0 Maoni