Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi imepiga hatua katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi baada ya kukamilisha ujenzi wa majengo sita ya kutolea huduma za afya katika Kituo cha Afya Katuma.
Ujenzi wa majengo hayo umegharamiwa kupitia fedha zinazotokana na Biashara ya Kaboni katika vijiji vya Katuma, Kapanga na Mpembe, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya kijamii inayolenga kuhakikisha jamii inanufaika moja kwa moja na shughuli za uhifadhi wa mazingira.
Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 700 unalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa Kata ya Katuma na maeneo jirani, huku ukidhihirisha umuhimu wa uhifadhi wa mazingira katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, katika Kata ya Katuma, Oktoba 18, 2026, Katibu wa Kamati ya Ujenzi na Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Bw. Pascal Masobeji, amesema ujenzi huo umekamilisha majengo muhimu yanayohitajika katika utoaji wa huduma za afya.
Masobeji amesema Kata ya Katuma ilipokea fedha hizo kwa awamu mbili. Katika awamu ya kwanza, iliyohusisha mgao wa awamu ya nne na ya sita, kata ilipokea Shilingi milioni 168 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD).
Amesema utekelezaji wa mradi huo umeimarisha ushirikiano kati ya Kata ya Katuma na vijiji vinavyonufaika na Biashara ya Kaboni, huku ukionesha namna mapato yatokanayo na uhifadhi wa mazingira yanavyoweza kuelekezwa katika miradi ya kijamii yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Katuma wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kuwezesha jamii kunufaika na Biashara ya Kaboni.
Wamesema kukamilika kwa majengo hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya katika eneo hilo, huku wakitarajia kuwa mradi huo utasaidia kupunguza changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Aidha, Waziri Masauni ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuhifadhi mazingira na kutumia vizuri Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kwa ajili ya kusajili miradi pamoja na kupata elimu kuhusu Biashara ya Kaboni.
“Serikali itaendelea kusimamia ili kuona jamii inanufaika na miradi hii, kwa kuwa Wilaya ya Tanganyika imekuwa mfano wa kuigwa katika Biashara ya Kaboni na imefungua njia kwa wengine kufanya biashara hii,” amesema Waziri Masauni.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia mgawanyo wa mapato yatokanayo na Biashara ya Kaboni ili kuhakikisha jamii zinaendelea kunufaika, sambamba na kuhamasisha wananchi kuendelea kulinda na kutunza mazingira.
Utekelezaji wa mradi huo unaendelea kutoa picha ya namna uhifadhi wa mazingira unavyoweza kuwa chanzo cha maendeleo ya jamii, hususan pale mapato yatokanayo na Biashara ya Kaboni yanapoelekezwa katika huduma muhimu kama afya.

0 Maoni