Wakili wa familia ya Mushi, inayoshikiliwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay kwa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amemuomba mkuu huyo wa mkoa kuwaachilia wanafamilia hao wanaodaiwa kushikiliwa tangu Jumatatu, Septemba 21, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari, wakili wa familia hiyo, Wilson Ogunde, amesema anaamini Mkuu wa Mkoa alipatiwa taarifa za kupotoshwa kuhusiana na kutokuwepo kwa wanafamilia hao katika ziara yake iliyofanyika Jumapili, Septemba 20, 2026.
Ogunde amesema wanafamilia hao walikuwa Moshi, mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara hiyo na hawakuwa na taarifa kuhusu ziara ya mkuu wa mkoa. Amesema walirejea Dar es Salaam kwa hiari baada ya kupata taarifa kuwa Mkuu wa Mkoa alitoa agizo la kutakiwa kufika kwa ajili ya kutoa maelezo kuhusu mgogoro wa ardhi unaohusisha familia mbili za David Moshi na Mariam Mongi.
“Wanafamilia hao walikuwa Moshi, mkoa wa Kilimanjaro wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa Chalamila siku ya jumapili Sepemba 20, 2026 na wala hawakuwa na taarifa yoyoye ya ziara hiyo ya mkuu wa mkoa,” alisema Ogunde.
Amesema siku moja kabla ya ziara hiyo, familia hizo ziliitwa katika kikao katika Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi kwa ajili ya usuluhishi wa mgogoro huo. Kikao hicho, kwa mujibu wa Ogunde, kiliongozwa na Kamishna Kyando akishirikiana na maofisa wa ardhi na wanasheria na kilidumu hadi saa 12 jioni.
Ogunde amesema baada ya kikao hicho, baadhi ya wanafamilia waliomba ruhusa kurejea Moshi mkoani Kilimanjaro ambako ni makazi ya baadhi yao, huku wakitarajia kuendelea na shughuli zao nyingine.
Amesema baadaye familia hizo zilipata taarifa kupitia mitandao ya kijamii kwamba Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila alikuwa ametoa agizo la wanafamilia wote kukamatwa, jambo lililowafanya kurejea Dar es Salaam kwa hiari na kufika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kutoa maelezo.
Hata hivyo, amesema hawakufanikiwa kuonana na Mkuu wa Mkoa na badala yake walipewa maelekezo ya kufika Kituo cha Polisi Oysterbay, ambako waliripoti kwa kufuata maelekezo hayo.
Wakili huyo amesema baada ya kufika kituoni hapo, wanafamilia hao walishikiliwa, wakiwemo bibi wawili na vijana watatu. Amesema katika yao yupo bibi mwenye umri wa miaka 86 anayehitaji huduma maalumu za afya na kwamba hadi sasa wanafamilia hao bado wanashikiliwa.
Ogunde amesema familia hiyo imekuwa ikishirikiana na mamlaka kila ilipoitwa katika vikao vya kutafuta suluhu ya mgogoro huo, na kwamba hakuna wakati ilipokataa kufika au kutoa ushirikiano.
“Familia hizi zimepata ushindi mahakamani na ni wamiliki halali wa maeneo hayo. Kwa msingi huo, tunaamini hawapaswi kusumbuliwa kwa sababu ya kudai au kulinda mali yao ambayo tayari suala lake limefanyiwa uamuzi na Mahakama,” amesema Ogunde.
Amesema wanafamilia hao wanaamini kuwa hawakutenda kosa lolote na walifika Dar es Salaam kwa hiari baada ya kupata taarifa za agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Tunamuomba Mkuu wa Mkoa aagize kuachiliwa mara moja kwa wanafamilia hawa ambao hadi sasa bado wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay,” amesema Ogunde.
Aidha, ameiomba Jeshi la Polisi kuzingatia haki za kikatiba za watu wanaoshikiliwa, ikiwemo kuzingatia hali zao za kiafya na kuhakikisha wanashikiliwa kwa mujibu wa sheria.
Ogunde amesema familia inaamini kuwa mamlaka zinapaswa kutumia njia za kisheria katika kushughulikia mgogoro huo, huku zikizingatia hatua zilizokwisha kuchukuliwa katika mchakato wa kutafuta suluhu.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliagiza familia ya David Mushi kukamatwa na kuhifadhiwa kwenye Kituo cha Polisi cha Oysterbay hadi siku ya Jumatatu, Septemba 21, baada ya kudharau wito wake alipotembelea eneo la Mtaa wa Madale wilayani Kinondoni lililokuwa na mgogoro wa ardhi baina ya familia hiyo na familia ya Abdallah Msham Kitwanga.
Chalamila alitoa maelekezo hayo mara baada ya kufika kwenye eneo hilo la wananchi zaidi ya kaya 15 walioathiriwa na mgogoro wa ardhi unaohusisha familia za marehemu Abdallah Msham Kitwanga na marehemu David Mushi katika Mtaa wa Madale wilayani Kinondoni, ambao waliondoshwa kwenye nyumba zao na kutolewa vyombo vyao nje tangu Septemba 3 mwaka huu kufuatia familia ya David Mushi kupata ushindi wa kesi ya mgogoro huo mahakamani, lakini familia hiyo ya Devid Mushi haikutii kuwepo eneo hilo.
Akizungumza mara baada ya kufika kwenye eneo hilo la mgogoro, Chalamila amesema alitoa taarifa ya kufika kwenye eneo hilo ili akutane na familia zote mbili za mgogoro huo pamoja na wahanga, lakini familia ya David Mushi imedharau wito huo huku akisisitiza kuwa hakuwa na mpango wa kuvunja hukumu iliyotolewa na mahakama, bali alitamani kuwakutanisha ili kama itawezekana kuwe na maridhiano ya wananchi kuweza kununua maeneo hayo.

0 Maoni