Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Mwang’onda amempongeza Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini Wilaya ya Muleba, Mhandisi Dativa Telesphory kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri hiyo.
Mwang’onda alitoa pongezi hizo wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru wilayani Muleba, akibainisha kuwa usimamizi madhubuti ni msingi muhimu wa kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali zinatumika ipasavyo na kuleta tija inayotarajiwa kwa wananchi. Alisema Mhandisi Dativa, ambaye pia ni Mratibu wa Mwenge wa Uhuru wilayani humo, ameonesha mfano mzuri wa jinsi wataalamu wanavyoweza kutumia taaluma zao kuchochea maendeleo, huku akitoa wito kwa wahandisi wengine kujitoa kimasomaso kusaidia wilaya hiyo kusonga mbele katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na majengo.
Aidha, Mwang’onda amewasihi viongozi wa serikali wilayani Muleba kuendelea kuwa wasimamizi wazuri wa miradi ili kuhakikisha rasilimali zinazotolewa na serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinaleta thamani halisi na manufaa yanayoonekana kwa wananchi.

0 Maoni