Serikali Yachukua Hatua Kushusha Bei ya Saruji

Serikali imetoa agizo la kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kudhibiti na kupunguza bei ya mfuko wa saruji ambayo imekuwa ikipanda hadi kufikia shilingi 27,000, 30,000 na hata 32,000 katika baadhi ya maeneo.

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Lagangabili, Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, ambapo alieleza kuwa amepokea maelekezo maalum kutoka kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kutaka wananchi wapate bidhaa hiyo kwa bei nafuu na inayoeleweka.

Alisema kuwa amewapa wataalamu muda wa wiki moja pekee kukaa na kuandaa mpango mahususi utakaorejesha bei ya saruji katika hali yake ya kawaida ili kuondoa kilio cha wananchi, huku akibainisha kuwa serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu minyororo ya uzalishaji na usambazaji.

Wakati akifafanua changamoto hiyo ya saruji, Dk. Mwigulu aligusia pia maagizo yaliyotolewa hivi karibuni na viongozi wengine wa serikali, yakiwemo ya Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi, ambaye aliagiza Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukutana na wazalishaji ili kubaini mianya inayochochea kupanda kwa gharama hizo.

Takwimu za wizara zinazohusika zinaonyesha kuwa Tanzania ina viwanda 15 vya saruji vinavyozalisha kiasi kinachozidi mahitaji ya ndani kwa mwaka, jambo ambalo linaashiria kuwa kupanda kwa bei hakutokani na uhaba wa bidhaa bali kunachangiwa na changamoto za kiushindani, usambazaji na mbinu za wafanyabiashara wa kati wanaohifadhi bidhaa kwenye maghala.

Chapisha Maoni

0 Maoni