ORCI yaanza safari ya ithibati ya kimataifa, yalenga kuongeza ubora, usalama na imani ya wagonjwa

Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) imeanza maandalizi ya kupata ithibati ya ubora wa huduma ikiwa tayari imefanya tathmini katika maeneo mbalimbali na kubaini mapungufu yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kufikia viwango vya ubora vinavyotambulika kimataifa.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za ORCI za kuimarisha mifumo ya utoaji huduma, kuongeza usalama wa wagonjwa na kuhakikisha huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo zinaendana na viwango vya ubora vinavyokubalika kimataifa.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi Tiba na Uhakiki Ubora wa ORCI, Hemed Myanza wakati akieleza hatua zilizofikiwa katika mchakato wa kupata ithibati, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi katika kikao cha sita cha baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Stella Maris wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Myanza alisema  katika maandalizi hayo ORCI imeweka mkazo katika kuhakikisha Taratibu za Kawaida za Uendeshaji (Standard Operating Procedures – SOPs) zinawekwa na kutumika katika maeneo yote ya taasisi ili kuwepo kwa mifumo na viwango vinavyofanana katika utoaji wa huduma.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila eneo la huduma linafanya kazi kwa kuzingatia taratibu na viwango vilivyowekwa jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi, usalama na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wagonjwa.

Aidha Myanza alisema  ORCI tayari imefanya mazungumzo na bodi zinazohusika na ithibati za kimataifa hatua inayolenga kusaidia taasisi kubaini chombo cha ithibati itakachoshirikiana nacho pamoja na kuelekezwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kufikia kiwango cha kupata ithibati ya kimataifa.

"Tumeshatoa elimu kwa wafanyakazi na tumeweza kuona maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia maboresho. Tumekwenda katika maeneo yote ya kitabibu na yasiyo ya kitabibu ili kuhakikisha watumishi wanakuwa na uelewa mmoja kuhusu viwango vinavyotakiwa kimataifa katika utoaji wa huduma," alisema Myanza.

Alisema mchakato huo haujajikita katika maeneo ya kitabibu pekee bali unahusisha pia maeneo yasiyo ya kitabibu ili kuhakikisha watumishi wote wanakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu viwango vinavyopaswa kuzingatiwa katika utoaji wa huduma.

Myanza alisema  huduma kwa wateja (customer care) ni miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele katika mchakato huo, ambapo ORCI inalenga kuhakikisha watumishi wanakuwa na uelewa na uwezo wa kutoa huduma bora, salama na zenye viwango vya juu vinavyoweza kuendana na viwango vya kimataifa.

Alisema  tathmini zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ya taasisi zimewezesha kubaini mapungufu yanayohitaji kufanyiwa kazi huku hatua za maboresho zikiendelea ili ORCI iweze kufikia viwango vinavyohitajika.

"Lengo la ithibati ni kuhakikisha taasisi inatambuliwa kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa. Tumefanya tathmini na kubaini maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia maboresho ili kufikia viwango hivyo vya kimataifa." alisema.

Myanza alisema kupata ithibati hiyo kutasaidia kuongeza imani na uaminifu wa wagonjwa kwa ORCI kwa kuwa utambuzi huo utaonesha kuwa taasisi inatoa huduma kwa kuzingatia viwango vinavyotambulika vya ubora na usalama.

"Tunatarajia ithibati hii itaongeza imani na uaminifu wa wagonjwa kwa sababu watakuwa na uhakika na kuthamini zaidi huduma wanazozipata katika taasisi yetu," alisema.



Chapisha Maoni

0 Maoni