Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni, Ofisi ya Makamu wa Rais imetoa mafunzo kuhusu Udhibiti wa Uingizaji wa Kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal.
Mafunzo hayo yametolewa jijini Dar es Salam leo Septemba 16, 2026 kwa maafisa wa Serikali waliopo katika Bandari ya Dar es salaam na Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere yakilenga kuwaongezea uelewa na uwezo kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa kemikali hizo.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa alitoa wito kwa washiriki hao kuendelea kuwajibika katika kusimamia ulinzi wa tabaka la ozoni.
Alisema maafisa wa forodha, wasimamizi wa sheria na maafisa wengine katika maeneo ya bandari na viwanja vya ndege wana wajibu muhimu wa kutambua, kukagua na kudhibiti uingizaji wa bidhaa mbalimbali, ikiwemo kemikali na vifaa vyenye kemikali zinazodhibitiwa.
“Warsha hii ni muhimu kwasababu inawalenga Maafisa wa Serikali wanaotekeleza majukumu katika maeneo ambayo ni lango kuu la kuingiza bidhaa nchini,” alisisitiza.
Akizungumzia umuhimu wa Tabaka la ozoni, Bi. Kemilembe alisema lina jukumu muhimu katika kulinda uhai duniani kwa kuchuja sehemu kubwa ya mionzi hatarishi ya urujuani kutoka kwenye jua kabla haijafika kwenye uso wa dunia.
Alisema uharibifu wa tabaka hili unaweza kuongeza kiwango cha mionzi hiyo kinachofika duniani na hivyo kuongeza hatari kwa afya ya binadamu, ikiwemo kuongezeka kwa magonjwa ya ngozi, madhara ya macho na kudhoofika kwa kinga ya mwili. Aidha, uharibifu wa tabaka la ozoni unaweza kuwa na madhara kwa mifumo mbalimbali ya ikolojia na ukuaji wa mimea.
Vilevile, baadhi ya kemikali zinazohusishwa na uharibifu wa tabaka la ozoni zina uwezo wa kuchangia ongezeko la joto duniani na hivyo kuongeza changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
Hivyo, aliwataka washiriki hao kuwa mabalozi wa elimu kuhusu uhifadhi wa tabaka la ozoni katika taasisi zao na kwa wadau wengine.

0 Maoni