Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson, amesema kuwa ushawishi mkubwa wa Tanzania katika duru za kimataifa pamoja na heshima iliyonayo vimesadia kwa kiasi kikubwa nchi kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa IPU utakaofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026.
Mkutano huo pia utachagua Rais ajaye wa umoja huo .
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa na kituo cha TBC1, Dk. Tulia alieleza kuwa misingi thabiti
iliyoachwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, katika kusimamia misimamo ya amani, mazungumzo, na maazimio, imeongeza uaminifu na heshima ya nchi duniani kote.
Alibainisha kuwa katika uongozi wake wa miaka mitatu kama Rais wa IPU, anajivunia kusimamia msimamo huo wa kitanzania pamoja na kufanya marekebisho ya katiba na sheria za umoja huo ambazo zimewezesha hoja nyingi kujadiliwa kwa wakati mmoja, tofauti na hapo awali ambapo utaratibu ulikuwa ukizuia hoja za bara la Afrika na nchi zinazoendelea kupata nafasi ya kutosha kutokana na changamoto za upigaji kura.
Dk. Tulia aliongeza kuwa kupata uenyeji wa mkutano huo mkubwa wa dunia si jambo la bahati mbaya, bali umoja huo huangalia kwa kina uwezo wa nchi katika kupokea wageni, utayari wa miundombinu ya malazi na chakula, pamoja na utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayosimamiwa na IPU kiutendaji.
Alifafanua kuwa mafanikio ya uongozi wake yamegusa maeneo mtambuka yakiwemo ya kukuza amani duniani, kusimamia haki za binadamu na wabunge, kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuhimiza matumizi ya sayansi na teknolojia bungeni ili kupunguza matumizi ya makaratasi.
Akizungumzia maandalizi yanayoendelea nchini kwa ajili ya mkutano huo wa kihistoria, alieleza kuwa Bunge la Tanzania chini ya Spika Mussa Zungu limeunda kamati maalum za ufuatiliaji zitakazosimamia masuala ya chakula, malazi, na mapokezi ya wageni ili kuhakikisha kila kitu kinakaa vizuri na kuipa sifa nzuri nchi.
Alisisitiza kuwa serikali na Bunge zimeweka mikakati thabiti ya kuwashawishi wageni hao zaidi ya elfu kadhaa watakaohudhuria mkutano huo kuona vivutio vya kipekee vya kitalii vilivyopo nchini, kujifunza tamaduni za kitanzania, na kushuhudia ukarimu wa wananchi, huku akibainisha kuwa serikali imeweka urahisi maalum ikiwemo utaratibu wa wageni kupewa vibali vya kuishi nchini bure pindi wanapowasili.
Alisema kuwa mkutano huo utakuwa fursa adhimu kwa Tanzania kuendelea kuitangaza nchi kimataifa, kuimarisha sekta ya utalii, na kuonyesha uwezo wake wa kuongoza na kuratibu matukio makubwa ya kimataifa yenye tija kwa ustawi wa dunia.

0 Maoni