Rais Samia ahitimisha Tamasha la Kizimkazi kwa kukaribisha uwekezaji zaidi

 

Na. Bakari S. Machumu- Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewakaribisha wawekezaji kutumia fursa zinazoendelea kukua mkoani Kusini Unguja, kufuatia maendeleo ya miundombinu, huduma za jamii na shughuli za kiuchumi. 

Akihutubia katika kilele cha Tamasha la Kizimkazi 2026 leo, tarehe 14 Agosti 2026, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Wilaya ya Kusini imebadilika kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni, ikichochewa na ongezeko la uwekezaji na miradi ya maendeleo. 

Rais Dkt. Samia amesema fursa hizo, pamoja na uwekezaji katika miundombinu, zimeendelea kuvutia shughuli mpya za kiuchumi, akisisitiza wajibu wa viongozi kuhakikisha uwekezaji huo unaacha manufaa ya kudumu kwa wananchi. 

Aidha, ametoa rai kwa wawekezaji kutumia fursa mpya zitakazoambatana na ujenzi wa uwanja wa michezo Kusini Unguja, unaotarajiwa kutumika katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika. 

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amewataka wananchi kuendelea kulinda amani, umoja, usalama na utulivu wa nchi, akibainisha kuwa shughuli za uwekezaji, utalii, biashara, ajira na huduma za jamii haziwezi kustawi katika mazingira ya vurugu. 

“Amani ndiyo kila kitu katika maisha yetu,” amesema Rais Dkt. Samia, akiwataka Watanzania kudumisha umoja na kuuenzi Muungano kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amelitaja tamasha hilo kuwa jukwaa muhimu la kutangaza Kizimkazi, kuhifadhi mila na utamaduni na kuchochea maendeleo. 

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia utunzaji na uendelezaji wa miradi iliyotokana na Tamasha la Kizimkazi ili iweze kudumu na kutoa huduma kwa wananchi. 

Akiwasilisha salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, amesema uwekezaji uliofanyika katika miaka ya hivi karibuni umeibadilisha Kizimkazi na kunufaisha makundi mbalimbali ya wananchi. 

Ametaja sehemu ya mafanikio hayo kuwa elimu ya usimamizi na mitaji kwa wajasiriamali wadogo kutoka taasisi za fedha nchini, fursa katika biashara ya utalii kwa vijana, pamoja na kupanuka kwa shughuli za uvuvi zilizoletwa na uwekezaji katika uchumi wa buluu. 

Tamasha la Kizimkazi, lililoanzishwa mwaka 2016, limepanuka na kuwa jukwaa linalounganisha miradi ya maendeleo, biashara, uwekezaji, michezo, utalii na shughuli za kijamii Kusini Unguja. 

Kupitia tamasha hilo, miradi mbalimbali ya maendeleo iliwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa katika sekta za elimu, afya, maji, barabara, makazi, burudani na michezo, huku shughuli zake zikivuta wafanyabiashara, wawekezaji na wageni kutoka Zanzibar, Tanzania Bara na nje ya nchi. 

Sherehe hizo, sambamba na washiriki wengine, zilihudhuriwa pia na wageni kutoka nje ya nchi, akiwemo Rais wa zamani wa Jamhuri ya Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embaló.






Chapisha Maoni

0 Maoni