Tamasha la Sanjo ya Busiya lasisitiza amani

 

Chifu wa Tatu wa Sanjo, Chifu Faustine Makwai, amesema Tamasha la Sanjo ya Busiya ni nyenzo muhimu ya utamaduni inayosisitiza upendo na kuwa wamoja.

Aidha amewataka wananchi kuendeleza mila na desturi zao pamoja na kudumisha amani.

Kauli hiyo ya kihistoria iliambatana na milio ya ngoma katika Kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, ambapo tamasha hilo la 16 liligeuka daraja la kipekee lililowaleta pamoja wananchi na machifu kutoka ndani na nje ya nchi, zikiwemo nchi za Kenya na Afrika Kusini, waliojitokeza kushuhudia na kuenzi urithi huo mwanana wa Kiafrika.

Mshikamano huo wa kitamaduni ulikolezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ambapo alipongeza jinsi sherehe hizo zilivyowaunganisha Watanzania kusherehekea siku ya Sabasaba kwa amani na kudhihirisha kuwa wao ni damu moja wanaopaswa kushirikiana katika kazi na maendeleo.

Wakazi wa Kishapu, akiwemo Bugali Mbushi, waligubikwa na tabasamu huku wakikiri kuwa tamasha hilo limewajenga kuwa wamoja na kuwapa nguvu mpya ya kulinda na kuendeleza utamaduni wao usipotee.

Chapisha Maoni

0 Maoni