Na.
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amewataka Waandishi wa Habari nchini kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa weledi, uzalendo na maadili ya taaluma, akisisitiza kuwa kalamu wanayoitumia ina nguvu kubwa ya kujenga au kubomoa taifa kupitia taarifa wanazozifikisha kwa umma.
Bw. Msigwa ametoa
wito huo tarehe 08 Julai, 2026 alipotembelea banda la Bodi ya
Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) katika Maonesho ya 50 ya
Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), akisema waandishi
wa habari wana nafasi ya kipekee katika kuhamasisha maendeleo ya
taifa na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia taarifa zenye ukweli,
usahihi na maslahi mapana ya nchi.
Alisema waandishi wa habari
wa zamani walifundishwa kuwa kalamu ni chombo chenye nguvu kubwa
kuliko silaha kwa sababu inaweza kuathiri fikra, maamuzi na mwelekeo
wa jamii.
“Kwa sisi tuliosoma habari zamani tunajua kuwa
kalamu ni hatari kuliko bunduki. Kalamu inaweza kuua kundi kubwa la
watu, huku risasi ikiua kulingana na idadi ya risasi zake,” alisema
Msigwa.
Aidha, aliwataka Waandishi wa Habari kujiepusha na
kile alichokiita habari za kikasuku zinazorudia simulizi bila
uchambuzi wa kina wala uhakiki wa taarifa, akisema mwenendo huo
unadhoofisha taaluma ya habari na hauchangii maendeleo ya
nchi.
“Tuepuke habari za kikasuku na waandishi wanaobagaza
nchi yao. Tuwe na waandishi wanaosikiliza, wanaochambua na kueneza
mema ya nchi yao ili kukuza uchumi,” alisisitiza Msigwa.
Msigwa
alitumia fursa hiyo kuipongeza Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa
Habari (JAB) kwa hatua kubwa iliyofikia katika kusajili, kuthibitisha
na kutoa vitambulisho vya ithibati kwa Waandishi wa Habari nchini.
Alisema taarifa ambazo Wizara imekuwa ikipokea zinaonesha
kuwa utekelezaji wa jukumu hilo umepokelewa vizuri na wadau wa sekta
ya habari, huku Waandishi wa Habari wengi wakionesha kuridhishwa na
huduma zinazotolewa na Bodi huku akiwasisitiza waandishi wa Habari
ambao bado hawajajisajili kuhakikisha wanapata ithibati kwa kuwa ni
takwa la kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari.
Akitoa
taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesema hadi sasa zaidi ya Waandishi
wa Habari 4,500 wamejisajili katika mfumo wa Bodi, ambapo kati yao
zaidi ya 3,650 tayari wamepatiwa ithibati na vitambulisho
vinavyowawezesha kutekeleza shughuli zao kwa mujibu wa sheria.

0 Maoni