Vijana watakiwa kutumia Saccos na Ushirika kujikwamua kiuchumi

 

Waziri wa Vijana, Joel Nanauka, amewahimiza vijana nchini kujiunga na mifumo rasmi ya kiuchumi kupitia vikundi, Saccos, vyama vya ushirika na biashara zilizosajiliwa ili kujiongezea fursa za kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Nanauka alitoa wito huo wakati wa uzinduzi wa tawi la Benki ya Coop Morocco jijini Dar es Salaam, akisema ushiriki wa vijana katika mifumo rasmi ya kifedha utawasaidia kujenga historia nzuri ya kifedha, kupata masoko ya bidhaa na huduma pamoja na kuimarisha biashara zao.

Amesema hatua hiyo pia itawawezesha vijana kukidhi vigezo vya kupata mikopo na huduma nyingine zinazotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa kundi hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Coop, Godfrey Ng'urah, amesema dhamira ya benki hiyo ni kutatua changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa wananchi wengi kupitia kukuza ujumuishi wa kifedha.

Ng'urah amesema benki hiyo itaendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi ili kuwawezesha kupata huduma za kifedha kwa urahisi zaidi na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Abdulmajid Nsekela, amesema lengo la sekta ya ushirika ni kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia watu wengi zaidi na kuwapa fursa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.



Chapisha Maoni

0 Maoni