Baraza la Vyama vya Siasa lahimiza mazungumzo yenye staha kulinda amani ya taifa

 

BARAZA la Vyama vya Siasa nchini limeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufungua nafasi ya majadiliano na mashauriano kati ya wadau wa kisiasa, hatua iliyotajwa kusaidia kulinda umoja, amani na mshikamano wa taifa.

Akitoa taarifa ya maazimio ya kikao cha siku tatu cha baraza hilo kilichomalizika Juni 18, 2026 mjini Morogoro, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib alisema wajumbe wamekubaliana kuendelea kuhimiza mazungumzo yenye staha na kuepuka kauli zinazoweza kuleta mgawanyiko nchini.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe kutoka vyama 18 kati ya 19 vyenye usajili kamili, wakiwemo wenyeviti wa vyama, makatibu wakuu, viongozi wa wanawake na wajumbe wengine waalikwa.

Khatib alisema baraza lina imani kuwa Tanzania itaendelea kuwa nchi moja, yenye umoja na mshikamano.

Alisisitiza kuwa baraza hilo linaipongeza serikali kwa kufungua milango ya mashauriano, na akatoa wito wa kuendelea kujenga maridhiano huku wakiepuka lugha zinazoweza kuwagawa wananchi.

Aliongeza kuwa baraza limebaini kuwepo kwa baadhi ya kauli kutoka kwa viongozi wa kisiasa ambazo hazijengi umoja wa taifa na kuwataka viongozi wote kuzingatia maadili ya uongozi kwa maslahi mapana ya nchi.

Aidha, alisema jukumu la baraza ni kuishauri serikali kwa lugha ya staha na kwamba serikali imeendelea kuonesha usikivu kwa kupokea na kufanyia kazi ushauri unaotolewa, hususan katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Awali, akifungua warsha hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuwa mabalozi wa amani, umoja na utulivu.

Chapisha Maoni

0 Maoni