SERIKALI imeeleza mpango wa kuongeza fursa za elimu ya juu nchini kwa kuongeza idadi ya wanafunzi watakaonufaika na mikopo, hatua inayolenga kukabiliana na ongezeko la wahitimu wanaojiunga na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, bungeni jijini Dodoma Mei 7, 2026, alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Prof. Mkenda amesema Serikali itaendelea kuratibu udahili wa wanafunzi takriban 180,000 wanaotarajiwa kuomba kujiunga na programu mbalimbali za shahada ya kwanza katika vyuo vya elimu ya juu nchini, sambamba na kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanapata mikopo kwa wingi zaidi.
Ameeleza kuwa idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu itaongezeka kutoka wanafunzi 252,773 katika mwaka wa fedha 2025/2026 hadi kufikia 292,981 mwaka 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua upatikanaji wa elimu ya juu.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada 24,978 katika fani za sayansi na ufundi, hatua inayolenga kuongeza rasilimali watu wenye ujuzi unaohitajika katika sekta za uzalishaji na teknolojia.
Ongezeko hilo la mikopo linatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha elimu ya juu inakuwa jumuishi zaidi, huku ikizingatiwa mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

0 Maoni