Serikali
imetangaza kuwa Mkoa wa Njombe unatarajiwa kuwa kitovu kipya cha
uwekezaji wa madini nchini baada ya kugunduliwa kwa madini adimu ya
Rare Earth Elements (REE) ya aina mbili ambayo ni Neodymium Nd na
Praseodymium Pr yenye mahitaji makubwa katika teknolojia za kisasa
duniani.
Akizungumza katika kijiji cha Mkiu Wilaya ya Ludewa,
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Lucas Mlekwa, amesema
utafiti wa madini hayo unaendelea kufanywa na kampuni ya Hongji
Mining Co. Ltd kwa kushirikiana na wazawa, huku soko kubwa la madini
hayo likiwa nchini China kutokana na ukuaji wa haraka wa sekta ya
viwanda na teknolojia.
Amesema madini ya REE yanatumika katika
utengenezaji wa betri za magari ya umeme, mitambo ya kuzalisha umeme
wa upepo pamoja na vifaa mbalimbali vya kielektroniki vinavyotumika
duniani kote.
“Mkoa wa Njombe unaendelea kufungua ukurasa
mpya wa maendeleo kupitia rasilimali hizi muhimu ambazo zina mchango
mkubwa katika mapinduzi ya teknolojia ya kijani duniani,” amesema
Mhandisi Mlekwa.
Ameeleza kuwa kampuni hiyo tayari
imekamilisha awamu ya kwanza ya utafiti na sasa ipo katika awamu ya
pili ya uchunguzi wa kina kabla ya kuanza uzalishaji rasmi katika
eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 280.
Kwa mujibu wa
Mhandisi Mlekwa, zaidi ya shilingi bilioni moja tayari zimelipwa kama
fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo, huku tathmini ya athari kwa
mazingira (EIA) ikiwa katika hatua za mwisho kukamilishwa kabla ya
shughuli za uzalishaji kuanza.
Akizungumzia utekelezaji wa
mradi huo, Mkurugenzi wa Hongji Mining Co. Ltd, Yahya Mohamed,
amesema kampuni imechagua kutumia teknolojia ya In Situ Leaching
ambayo inapunguza athari kwa mazingira kwa kutohusisha uchimbaji
mkubwa wa mashimo ya wazi wala migodi ya chini ya ardhi.
Amesema
matumizi ya teknolojia hiyo yatawezesha uchimbaji endelevu huku
yakilinda mazingira na jamii zinazozunguka eneo la mradi.
“Tunataka
kuona wananchi wa Njombe wanakuwa sehemu ya mafanikio ya mradi huu
kupitia ajira, fursa za biashara na ongezeko la mapato ya kiuchumi,”
amesema Mohamed.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza mchango wa
sekta ya madini katika uchumi wa Mkoa wa Njombe, kuchochea uwekezaji
mpya pamoja na kuiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na soko la
kimataifa la madini adimu ambalo linaendelea kukua kwa kasi duniani.


0 Maoni