Mradi mkubwa wa
uzalishaji wa kokoto uliopo mtaa wa Kambarage kata ya Njombe Mjini,
unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa kokoto na kuchochea shughuli za
kiuchumi na kuongeza mapato ya Serikali katika Mkoa wa Njombe.
Mradi
huo unaomilikiwa na mchimbaji mdogo wa madini ya ujenzi, Isaya
Boniface, umefungwa mtambo mkubwa wa kusaga kokoto wenye uwezo wa
kuzalisha zaidi ya tani 1,000 kwa siku kwa kushirikiana na kampuni ya
India ya Shree Sonal Earth Ltd iliyotoa usaidizi wa kitaalam katika
utekelezaji wake.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Boniface
amesema uwekezaji huo utamaliza changamoto ya upatikanaji wa kokoto
ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikisafirishwa kutoka mikoa ya Iringa,
Dodoma na Pwani, hususan Lugoba, kwa matumizi ya miradi mbalimbali ya
ujenzi mkoani Njombe.
Amesema mradi huo utasaidia kupunguza
gharama za ujenzi, kuongeza ajira kwa wananchi, kukuza mzunguko wa
fedha pamoja na kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo
inayohitaji kokoto kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake, Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Lucas Mlekwa, amesema mradi
huo ni miongoni mwa uwekezaji muhimu unaotarajiwa kuongeza mapato ya
Serikali kupitia madini ujenzi.
Amesema kutokana na uwezo wa
uzalishaji wa tani 1,000 za kokoto kwa siku, Serikali inatarajia
kukusanya zaidi ya shilingi milioni 2.3 kwa siku kupitia tozo za
mrahaba na ada ya ukaguzi, huku makadirio ya mapato ya mwaka
yakifikia kati ya shilingi milioni 400 hadi 600.
“Mkoa wa
Njombe unaendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa sekta ya ujenzi wa
miundombinu, makazi na miradi ya Serikali, hivyo uwepo wa mradi huu
utaongeza upatikanaji wa malighafi muhimu kwa utekelezaji wa miradi
hiyo,” amesema Mhandisi Mlekwa.
Aidha, amesema Serikali
chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka
mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo kwa kushirikiana na taasisi za
kifedha ili kuwawezesha kupata mikopo na vifaa vya
uzalishaji.
Mhandisi Mlekwa ameongeza kuwa miradi mikubwa ya
maendeleo inayotekelezwa mkoani Njombe, ikiwemo mradi wa kiwanda cha
chuma, itaongeza mahitaji ya kokoto na kufungua zaidi fursa za
uwekezaji katika sekta ya madini ya ujenzi.



0 Maoni