MKOA wa Njombe unatarajiwa kuwa kitovu kipya cha
uchumi wa madini nchini kufuatia uwekezaji mkubwa katika miradi ya
uchimbaji na uchakataji wa madini ya chuma inayolenga kufungua maelfu
ya ajira, kukuza biashara za ndani na kuongeza mapato kwa wananchi wa
Wilaya ya Ludewa.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe,
Mhandisi Lucas Mlekwa, amesema tayari moja ya miradi mikubwa
inayosimamiwa na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kwa kushirikiana
na kampuni ya kigeni imepata Leseni Kubwa ya Uchimbaji wa Madini
baada ya utafiti wa kina uliofanyika kati ya mwaka 2012 na 2013
kubaini uwepo wa zaidi ya tani milioni 126 za madini ya
chuma.
Amesema tafiti hizo pia zimeonesha uwepo wa madini
mengine yenye thamani kubwa yanayoambatana na chuma ikiwemo titanium
na vanadium, hatua inayoongeza thamani ya kiuchumi ya mradi huo kwa
Taifa.
“Kwa sasa tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha
makubaliano kati ya Serikali na wawekezaji, na tunatarajia ndani ya
mwaka mmoja utekelezaji rasmi wa mradi utaanza,” amesema
Mlekwa.
Kwa mujibu wa Mlekwa, mradi huo utahusisha shughuli
kuu mbili ambazo ni uchimbaji wa madini pamoja na ujenzi wa kiwanda
cha kisasa cha kuchakata chuma kitakachozalisha bidhaa mbalimbali
zitakazotumika katika sekta ya ujenzi na viwanda nchini.
Ameeleza
kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza ushiriki wa wazawa kupitia
utekelezaji wa sera ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya
Madini, ambapo wananchi watanufaika na fursa za ajira na biashara
zikiwemo huduma za ulinzi, usafirishaji, ugavi wa vifaa vya ujenzi,
huduma za migodini pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi
zinazozunguka miradi hiyo.
Aidha, amesema mradi wa chuma wa
Maganga Matitu unaosimamiwa pia na NDC kwa ubia na kampuni ya kigeni
umefikia hatua za mwisho za maandalizi baada ya mwekezaji kulipa
zaidi ya Shilingi bilioni 4.2 kama fidia kwa wananchi waliopisha eneo
la mradi huo, ambao una akiba inayokadiriwa kufikia tani milioni 45
za madini ya chuma.
Mlekwa ameongeza kuwa pamoja na miradi
hiyo, Wilaya ya Ludewa itanufaika na utekelezaji wa mradi wa
Mchuchuma wenye zaidi ya tani milioni 428 za makaa ya mawe kwa
ajili ya uzalishaji wa umeme, unaotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa
nishati kwa shughuli za uchimbaji na viwanda vya chuma
vitakavyojengwa wilayani Ludewa.
Amesema maendeleo hayo
yataifanya Njombe kuwa miongoni mwa maeneo muhimu zaidi nchini katika
sekta za madini, viwanda na nishati, huku yakitarajiwa kuongeza
mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na
maendeleo ya wananchi wa eneo hilo.

0 Maoni