Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye
Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, ametoa ufafanuzi mzito kupitia
mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),
akibainisha hatua zinazofuata baada ya ripoti ya tume kubaini kuwepo
kwa vikundi vilivyopanga na kufadhili ghasia za uchaguzi.
Profesa
Kabudi ameweka wazi kuwa kazi iliyofanyika na Tume ya Jaji Chande
ilikuwa ni kutafuta ukweli na ukusanyaji wa taarifa ambapo imebainika
wazi kuwa kuna kundi lililojipanga, likafadhili, na hata kukusanya
vijana kwenye makambi kwa ajili ya mafunzo ya uhalifu, na kusisitiza
kuwa watu hao hawawezi kuwa sehemu ya serikali bali ni kundi
linalofahamika.
Akifafanua
kuhusu hatua za kisheria, Profesa Kabudi amesema kuwa baada ya
kukamilika kwa kazi hiyo ya kutafuta ukweli, sasa hatua inayofuata ni
upelelezi wa kina ambapo wale wote waliohusika lazima wapewe haki yao
ya kuitwa mbele ya vyombo vya upelelezi ili kujibu tuhuma
zinazowakabili.
Amesema kuwa hiyo ndiyo kazi ya msingi ya
upelelezi na hakuna mhusika atakayekwepa mkono wa sheria kwani
utambulisho wao uko wazi na ni lazima hatua zichukuliwe kwa mujibu wa
sheria za nchi.
Waziri huyo amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo, nchi itakuwa ikitekeleza mambo matatu makubwa kwa mpigo ambayo ni upelelezi kwa waliofanya makosa, mchakato wa maridhiano, na maandalizi ya Katiba Mpya.
Amefafanua kuwa Tume ya Maridhiano itaundwa kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini ili kuhakikisha ushirikishi wa kila mwananchi, huku akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina utashi mkubwa wa kisiasa wa kuhakikisha mchakato huo unafanikiwa na kuleta utulivu wa kudumu.
Kuhusu suala la Katiba Mpya, Profesa Kabudi ametoa matumaini makubwa kwa Watanzania akisema kuwa mahali pa kuanzia tayari papo na utashi wa Rais ni kielelezo tosha kuwa Katiba itapatikana.
Amesisitiza kuwa tume imependekeza Katiba hiyo mpya ipatikane ifikapo mwaka 2028, na akaongeza kuwa ikiwa wale wenye nia mbaya wataacha kuweka vitimbi na kuzuia mchakato huo, Watanzania watapata Katiba yenye matakwa yao na inayozingatia maslahi ya taifa kwa ujumla.
#UmojaWetuNdiyoNguvuYetu
#turidhiane

0 Maoni