Mwanasiasa , Odero Charles Odero, ametoa ushauri kwa Serikali kutunga sheria mahususi itakayosimamia mchakato wa maridhiano ya kitaifa ili kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi thabiti wa mazungumzo na utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa.
Akizungumza katika mahojiano na moja ya televisheni za mtandaoni
kuhusu mustakabali wa nchi baada ya kukabidhiwa kwa ripoti ya Tume ya
Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, Odero amesema anaikubali ripoti
hiyo na kuongeza kuwa maridhiano ya kweli hayawezi kupatikana kwa
mazungumzo ya hiyari pekee, bali yanahitaji mfumo wa kisheria
utakaotoa muongozo kama ilivyokuwa katika mchakato wa utafutaji wa
Katiba, akisisitiza kuwa "maridhiano yanapaswa kuanza na
sheria."
Odero ameeleza kuwa wakati umefika kwa Watanzania
kukaa katika makundi mbalimbali ili kuitafakari na kuijadili ripoti
hiyo kwa kina, kwa lengo la kutafuta namna bora ya kusonga mbele kama
taifa moja.
Amesisitiza kuwa katika majadiliano hayo, ni jambo la
msingi kwa wananchi na viongozi kutumia lugha ya staha, upendo, na
inayojenga badala ya kutumia lugha za chuki au uchochezi zinazoweza
kuligawa taifa.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, lugha njema ndiyo
msingi wa kuijenga Tanzania mpya yenye kuvumiliana, huku akionya kuwa
upinzani usio na tija hautasaidia nchi kujikwamua kutoka katika
changamoto ilizopitia.
Aidha, Odero ametoa rai kwa Serikali
kuangalia uwezekano wa kutoa fidia au faraja kwa familia zilizopoteza
wapendwa wao kama sehemu ya kuponya makovu na kurejesha matumaini kwa
waathirika wa matukio yaliyochunguzwa.
Amekiri kuwa ingawa ripoti
ya tume haiwezi kujitosheleza kwa asilimia mia moja, inapaswa
kutazamwa kama "mti unaoota na kukua" ambao unahitaji
maboresho ya mara kwa mara. Amewataka Watanzania kuangalia udhaifu
uliojitokeza kama fursa ya kufanya marekebisho na kuunga mkono juhudi
za maridhiano zinazopigania mshikamano wa taifa na amani ya kudumu.

0 Maoni