Mwanasiasa na
mwanadiplomasia wa kimataifa, Gertrude Mongela, ambaye amewahi
kuhudumu kama Rais wa kwanza wa Bunge la Afrika na Katibu Mkuu wa
Mkutano wa Nne wa Dunia wa Wanawake, anabainisha kuwa dunia ya sasa
inakabiliwa na changamoto kubwa ya lawama kati ya wazee na vijana.
Katika mahojiano Maalumu na BSKY Media, Mongela anasisitiza
kuwa sote kama binadamu tumetikiswa na mabadiliko ya tabia nchi,
uchumi, siasa, na teknolojia. Mabadiliko haya yanatupasa kujitathmini
upya ili kuendeleza jamii bila kusigana, kwani majadiliano ndiyo
msingi mkuu wa kupunguza hali ya sintofahamu na kutengeneza fursa za
kujitegemea.
Akilinganisha malezi ya zamani na ya sasa,
Mongela anabainisha kuwa uhusiano wa mzazi na mtoto umepungua
kutokana na mabadiliko ya kijamii. Anakumbuka jinsi zamani mtoto
alivyokuwa akilelewa mgongoni mwa mama yake, akihisi joto na upendo
wa moja kwa moja, tofauti na sasa ambapo watoto wengi hulelewa na
walezi wengine.
Hali kadhalika, alizungumzia mfumo wa mamlaka
ya baba nyumbani kuwa umeyumba; zamani baba alikuwa na sauti na kauli
iliyosimamiwa kwa nidhamu, jambo lililomfanya kijana kuwa na mipaka
na matumaini ya wazi kuhusu mustakabali wake. Leo hii, vijana
wanahitaji zaidi ya matumaini tu ili kukabiliana na ugumu wa maisha,
ikiwemo changamoto za mahusiano na ndoa ambazo zinahitaji jamii
kujitafakari upya.
Kuhusu mivutano kati ya vizazi, Mongela
anatoa onyo dhidi ya tabia ya wazee kuwalaumu vijana pekee, akisema
kuwa kufanya hivyo ni kuwaonea kwani hata baadhi ya wazee
"walishavurugwa."
Anasitiza umuhimu wa kutumia
busara badala ya lawama kwa kurejea kisa cha mzee mmoja huko Ukerewe
wakati akiwa mbunge ambaye alikiri kuwa, kama changamoto za sasa
(wakati huo katika mkutano wa hadhara walikuwa wanazungumzia ukimwi)
zingetokea wakati wa ujana wake, naye ugonjwa ungemkumba.
"Hii
inatufundisha kuwa badala ya kunyoosheana vidole, pande zote mbili
zinapaswa kukaa pamoja na kutumia fursa za majadiliano zilizopo ili
kupata utulivu na kusonga mbele kwa pamoja." alisema.
Akigusia
harakati za kudai uhuru na usawa, Mongela anatoa mifano ya wanawake
shujaa kama Binti Matola na Amina, ambao walitumia nguvu ya hoja na
ujasiri bila fujo kuleta mabadiliko.
Binti Matola alipinga
muda mrefu uliowekwa na wakoloni kwa kutumia mithali nzito, jambo
lililochochea vuguvugu la uhuru wa Tanzania kuwahi kufika mwaka 1961
badala ya 1971.
Mongela anafundisha kuwa ujasiri wa kweli si
kufanya fujo au vurugu, bali ni uwezo wa kufikiri na kusema kwa namna
inayoleta mabadiliko chanya. Anatoa wito kwa jamii kutumia majukwaa
yaliyopo kama makanisa, misikiti, na kamati za bunge kujadili ajenda
za kitaifa kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.
#KizaziChaAmani

0 Maoni