Kongamano la vijana, Shigongo aeleza maana ya uzalendo wa kweli

Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo amefafanua maana halisi ya uzalendo kwa vijana, akieleza kuwa uzalendo ni kuwa mwaminifu na mtiifu kwa nchi yako, si kwa mtu binafsi au taasisi, huku akisisitiza umuhimu wa kuipenda nchi na kuchangia maendeleo yake kwa vitendo.

Akizungumza katika Kongamano la Vijana, Shigongo amewahimiza vijana kutoikatia tamaa nchi yao, akibainisha kuwa Tanzania ni yao na wana wajibu wa kuilinda na kuiendeleza.

Amesisitiza kuwa kila kijana anapaswa kuona fahari kuwa sehemu ya taifa hili, akiongeza kuwa ni Mungu aliyewaweka hapa hivyo wanapaswa kuitumia nafasi hiyo kujenga mustakabali bora wao na wa nchi kwa jumla.

Aidha, ameeleza kuwa uzalendo wa kweli hauishii katika maneno pekee bali hujidhihirisha kupitia matendo kama kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia sheria za nchi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii. Amesema vijana wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko chanya endapo watatumia nguvu na vipaji vyao kwa manufaa ya taifa badala ya kusubiri msaada kutoka kwa wengine.

Pia amewataka vijana kuwa makini na upotoshaji unaoweza kuwakatisha tamaa kuhusu mustakabali wa nchi, akisisitiza kuwa kila changamoto inaweza kuwa fursa ya kujifunza na kujenga uwezo. Amesema kwa kushirikiana na kuwa na mshikamano, vijana wanaweza kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya Tanzania ya sasa na baadaye.

#MezaYaUmoja 

Chapisha Maoni

0 Maoni