Na. Baraka Serapion- Sweden
Aliyekuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, leo tarehe 14 Machi, 2026, amekutana na watumishi wa taasisi za utalii nchini kufuatia kukamilika kwa onesho la 'My Tanzania Roadshow 2026' lililofanyika katika nchi nne za Ulaya za Ujerumani, Denmark, Norway na Sweden.
Ziara hiyo ya kutangaza utalii wa Tanzania ilianza tarehe 8 Machi nchini Ujerumani na kuhitimishwa nchini Sweden tarehe 13 Machi, 2026 ikisimamiwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Ubalozi.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Matinyi aliwapongeza watumishi hao kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kuitangaza Tanzania katika soko la nchi za Ulaya Kaskazini, akieleza kuwa juhudi hizo ni muhimu katika kukuza sekta ya utalii na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
Aidha, alibainisha kuwa jitihada hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Serikali wa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania hadi kufikia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.
Akihitimisha mazungumzo hayo, Balozi Matinyi amewahimiza watumishi hao kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta ya utalii katika kuitangaza Tanzania kimataifa ili kuhakikisha vivutio vya nchi vinaendelea kufikia masoko mbalimbali ya utalii duniani.



0 Maoni