Ukiwa Umetoka Kuzini Usiingie Pango la Fatuma Kwenye Mapango ya Amboni Tanga

Ndani ya ardhi ya Tanga, palipo Mapango ya Amboni, kuna simulizi zisizoandikwa na historia, bali zinazoishi katika imani za vizazi. Miongoni mwa mapango hayo yapo yanayoheshimiwa na yanayotajwa miujizi ya aina yake likiwamo Pango la Fatuma.

Muongoza watalii katika mapango hayo Muhsini Juma anasimulia kuwa hili si pango la kawaida; ni eneo lenye masharti ya kimila na mipaka ya kiimani, ambapo mtu aliyeguswa na mahusiano ya kimwili haruhusiwi kuingia bila kujitakasa kwa kuoga. Kukiuka taratibu hizo, huaminika kufungua mlango wa mikosi, matatizo na misukosuko ya maisha.

Mwanaume akiingia kwenye pango hilo bila kuoga kuna uwezekano wa  kishindwa kufanya tendo la ndoa hadi hapo atakapokwenda kwa Wazee wa kimila na kusaidiwa na hivyohivyo kwa mwanamke akiingia bila kuoga kama ametoka kufanya mapenzi, mfumo wa mzunguko wa hedhi unaweza kuongeza siku tofauti na mzunguko za mwanzo aliouzoea.

Kwa miongo na karne, watu waliokata tamaa katika safari ya ndoa, waliokwama kuoa au kuolewa, wamekuwa wakielekea Amboni kwa matumaini mapya kuja kunong’ona majina ya wapendwa wao gizani, kutamka nia zao mbele ya nguvu zisizoonekana, na kuondoka wakiamini kuwa majibu yatakuja.

Muongoza watalii katika mapango hayo Muhsini Juma anaeleza kuwa watu wengi wamekuwa wakifanikiwa kupata wenza wao wanapofika katika pango la Fatuma ambalo limekuwa likitumika toka enzi za mababu kwa watu mbalimbali kufika na kuomba kupata mume au mke kwa kuishi nae kama mume na mke

“Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na changamoto sana ya vijana kupata wake au waume wa kuwaoa, lakini wakifika katika pango hili na kusema nia yao na kutambika  basi wanafanikiwa na kumekuwa na shuhuda nyingi za wadau ambao wamefanikisha jambo hilo na kurudi kutupa mrejesho,” alisema Muhsin.

Umaarufu wa pango hili umewafanya wageni kwa nyakati tofauti kutembelea na kujifunza jinsi ya kufanya matambiko hayo na baada ya muda si mrefu basi baadhi hurudi kwa ajili ya shukran na inaaminika kwamba si wenyeji tu wa mkoa wa Tanga wanaotembelea mahali hapo bali pia na watu katika maeneo mengine nje ya nchi.

Muhsin anaeleza kuwa ukifika katika pango la Fatuma kama una mtu ambaye unataka kumuoa au kukuoa basi unataja jina lake na kumuita na haitochukua muda mrefu mtu huyo mwenyewe ataanza kukutafuta kwa lengo la kutaka kuoa au kuolewa.

Na kwa wale ambao hawana mtu kabisa wakifika katika mapango hayo wanachotakiwa kusema ni kwamba mimi mwaka huu nataka kuoa au kuolewa na namkusudia mtu flani, mwenye sifa Fulani... haichukui muda mrefu wanapata wenza wa kufunga nao ndoa.

Pango hili la Fatuma ambalo ni miongoni mwa mapango yaliyopo Amboni pia linatumika kwa kufanya matambiko yanayohusu masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kupata mtoto, kuombea mvua inyeshe, kupata kazi na mambo mengine na ndiyo maana ukifika katika pango hilo watu kadhaa wa kadhaa hufanya maombi yao na mara nyingi hawataki waonekane zaidi ya kufuata taratibu za wenyeji wao kw autulivu na faragha.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeweka utaratibu mahsusi wa kuhakikisha kuwa jamii ya mkoa wa Tanga na wale ambao bado wanaamini mambo hayo wanapata wasaa wa kufanya matambiko yao bila kuathiri utamaduni huo uliopo miaka na miaka.

Hayo ndiyo maajabu ya pango la Fatuma na hii inadhihirisha kwamba mwenda tezi na omo marejeo ngamani, Amboni ndiyo ngama yako ya kupata mume au mke ,usidharau mila kwani mdharau mila ni mtumwa.

Chapisha Maoni

0 Maoni