Amani ndio ngao, mshikamano ni daraja la maendeleo

KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni muendelezo wa hamasa ya kulinda tunu za Taifa, wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wameibuka na kutoa mwito mzito kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na utulivu kama kigezo namba moja cha ustawi wa kiuchumi na kijamii.

Kutoka mkoani Pwani hadi Simiyu, ujumbe umekuwa mmoja: Amani haina mbadala.

Akizungumza mjini Kibaha, fundi magari wa eneo la Maili Moja, Frimatus Mtenga, ameweka mkazo katika jukumu la wazazi ndani ya familia. Mtenga anaamini kuwa mbegu ya amani inapaswa kupandwa kuanzia ngazi ya kaya kwa kuwafundisha watoto kuepuka kufuata mkumbo unaoweza kupelekea uvunjifu wa utulivu.

“Wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto wao namna ya kutunza amani na kuacha kufuata mkumbo. Mshikamano ndio ngao yetu inayotufanya tuweze kufanya shughuli zetu na kujiletea maendeleo yetu na nchi yetu kwa ujumla,” alisisitiza Mtenga.

Kwa upande wake, Katibu wa Kitengo cha Matunda katika Soko la Loliondo, Kibaha, Amina Mwinyimvua, amewatahadharisha Watanzania dhidi ya ushawishi wa nje unaolenga kubomoa utulivu uliopo. Amina anabainisha kuwa wafanyabiashara wadogo ndio waathirika wakuu pindi amani inapotikiswa.

Aliongeza kuwa utamaduni wa amani nchini Tanzania ni urithi kutoka kwa viongozi waasisi, na ni wajibu wa kila mwananchi kuulinda. "Mambo ya vurugu hatujayazoea. Tunahitaji utulivu ili tufanye shughuli zetu za kila siku; tuhakikishe tunailinda hii amani kwa maendeleo ya nchi yetu," alisema Amina.

Hali kadhalika, mdau wa sekta ya usafirishaji na mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu, Malugu Nkwabi, alikumbusha madhara ya kivitendo yanayotokea pindi amani inapopotea, hata kama ni kwa muda mfupi. Nkwabi alitoa mfano wa kipindi cha vurugu za uchaguzi ambapo mzunguko wa kiuchumi uliparaganyika na kuwalazimu watu kufunga shughuli zao mapema.

“Wakati wa vurugu, tulilazimishwa kufanya kazi hadi saa 12:00 jioni pekee. Yalikuwa ni maisha mapya na magumu sana kwetu. Vurugu zilitokea mikoa mingine, lakini adha yake ilitufikia sote,” alieleza Nkwabi huku akiwasihi vijana kutambua kuwa amani ndiyo kila kitu maishani.

Maoni ya wadau hawa yanathibitisha kuwa amani si suala la kisiasa pekee, bali ni hitaji la msingi la kiuchumi. Iwe ni fundi karakana, mama lishe sokoni, au dereva wa usafirishaji, wote kwa kauli moja wanakiri kuwa bila utulivu, gurudumu la maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla haliwezi kwenda mbele.

Chapisha Maoni

0 Maoni